Sehem Ya 1; Historia Ya Sewa Haji Paroo Mwanzilishi Wa Jengo La Hospitali Ya Muhimbili

Sewa Haji Paroo alijenga jengo la kutoa huduma za afya kwa watu mbalimbali.

KWA UFUPI
Alipokutana na Stanley alikuwa na miaka 20 tu, alizaliwa mwaka 1851.

Wasomaji kadhaa walitaka kujua zaidi kuhusu Sewa Haji Paroo anayetambulika kama mtu wa kwanza aliyejitolea kuanzisha huduma za afya na elimu kwa faida ya watu wote bila kujali rangi, daraja la kiuchumi wala dini ya mtu yoyote.

Ikumbukwe kwamba Bagamoyo kabla ya 1900 ulikuwa mji maarufu sana na makao makuu ya kwanza ya Serikali ya kikoloni yalikuwa katika mji huo chini ya Deutch Ost Africa. Watu wengi wakiwamo wazazi wa Sewa Haji walifika Bagamoyo kutoka pande mbalimbali za dunia kutafuta maisha.

Sewa Haji Paroo anatajwa na Henry Morton Stanley mpelelezi na mwandishi wa habari kutoka Marekani mwenye asili ya Uingereza kama Soor Hadji Paloo katika kitabu chake kuhusu safari ya Kumtafuta Dk David Livingstone.

Stanley alifika Bagamoyo akitokea Unguja Machi 1871 akiwa njiani kwenda Ujiji kumtafuta Livingstone na alielekezwa kumwona Soor Hadji (Sewa Haji) kwa ajili ya msaada wa kumtafutia wapagazi wa kumbebea mizigo hadi Ujiji; kumtafutia nguo, majora, vitenge na kaniki na sari na khaki tetroni.

Pia alikusanya shanga za aina mbalimbali ambazo zilikuwa zikitumika kama malipo kwa ajili ya kununulia mbuzi, mtama na vyakula vingine kwa ajili ya kuwalisha wapagazi. Soor Hadji, alitambulika pia kama mchuuzi mashuhuri wa biashara ya silaha ambazo alikuwa akiziagiza kutoka India. Wakati alipokutana na Stanley alikuwa na miaka 20 tu, alizaliwa 1851.

Wakati huo wamisionari na wapelelezi kama kina Livingstone, Burton, Speke na Stanley walikuwa wakihitaji bunduki kwa ajili ya ulinzi na kuwindia wanyama. Stanley anamweleza Soor Haji kama kijana mwenye unyenyekevu sana wa dini, lakini katika biashara alikuwa mwerevu sana na mwenye akili iliyokuwa ikifikiri kwa kasi sana.

Anamlaumu kuwa, katika kufanya biashara alikuwa mjanja kwa kupata zaidi ya Dola 1,300 za Marekani kutoka kwa Stanley peke yake. Soor Haji alinunua majengo Bagamoyo na Dar es Salaam na huko Mombasa kwa ajili ya kutumika kwa watu maskini.

Post a Comment

0 Comments