Na Humphrey Moris
Katika kipindi cha mabadiliko ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, moja ya mabadiliko yaliyozua mjadala mkubwa ni kuondolewa kwa January Makamba kutoka nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Uamuzi huu umekuwa na athari kubwa na una maswali mengi kuhusu sababu na malengo ya mabadiliko haya.
Mnamo tarehe 21 Julai 2024, Rais Samia alifanya mabadiliko kadhaa kwenye baraza lake la mawaziri, ikiwa ni pamoja na kumwondoa January Makamba na Naibu wake, Stephen Byabato, kutoka wizara hiyo. Nape Nnauye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, pia aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Jerry Silaa.
Mabadiliko haya yamechochea mijadala kuhusu sababu za Rais Samia kufanya uamuzi huu. Wachambuzi wa kisiasa wameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ni wizara yenye changamoto nyingi, na labda hii ndio sababu ya kuwa na mawaziri wanne tofauti katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.
Mawaziri hao ni:
- Prof. Palamagamba Kabudi: Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati Rais Samia alipoingia madarakani mwezi Machi 2021. Prof. Kabudi alihudumu hadi mwezi Mei 2021.
- Balozi Liberata Mulamula: Aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwezi Mei 2021 na alihudumu hadi Oktoba 2022.
- Dk. Stergomena Tax: Aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwezi Oktoba 2022 na alihudumu hadi mwezi Agosti 2023, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Huduma za Kitaifa.
- Januari Makamba: Aliteuliwa mwezi Septemba 2023 na kuondolewa madarakani mwezi Julai 2024.
Kuna nadharia na hoja nyingi zinazojaribu kuonyesha ni nini hasa sababu ya Januari Makamba na Nape Nnauye kuenguliwa. Walioenguliwa katika viti ni wengi, ila hoja ni watu hawa wawili ambao kihistoria wamewahi kupitia misukosuko kama hii na kutolewa kwenye nafasi zao si kwa uwezo wao mdogo bali migongano ya kisiasa.
Januari Makamba
Januari Makamba alikuwa Naibu Waziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini na Rais John Magufuli baada ya uchaguzi wa mwaka 2015. Hata hivyo, safari yake ya kisiasa ilipata changamoto kubwa wakati wa utawala wa Rais Magufuli.
Mnamo Julai 21, 2019, mawasiliano ya Januari Makamba, pamoja na mawasiliano ya viongozi wengine wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kama vile Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, yalidukuliwa. Mawasiliano hayo yalikuwa na maudhui ya kumkosoa Rais Magufuli na utawala wake. Katika mazungumzo hayo, Januari na viongozi wenzake walionekana kuzungumzia mapungufu ya uongozi wa Rais Magufuli, hali ambayo ilimuweka Januari katika nafasi mbaya kisiasa.
Baada ya kashfa hiyo, Januari Makamba aliondolewa kwenye baraza la mawaziri na Rais Magufuli.
Nape Nnauye
Nape alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia Desemba 2015. Mnamo Machi 2017, alifukuzwa katika nafasi hiyo baada ya mgogoro mkubwa kati yake na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Mgogoro huo ulisababishwa na kitendo cha Makonda kuvamia ofisi za Clouds Media Group akiwa na askari wenye silaha, akiwalazimisha kuonyesha taarifa ambazo Clouds hawakutaka kuzionyesha.
Nape alitaka Makonda achukuliwe hatua kwa kitendo hicho cha kutumia vibaya madaraka, lakini Rais Magufuli alimtetea Makonda, hali iliyosababisha mgongano kati ya Nape na Rais. Kwa sababu ya msimamo wake wa kudai hatua zichukuliwe dhidi ya Makonda, Nape aliondolewa kwenye baraza la mawaziri.
Urejeshaji wa Nafasi zao na Rais Samia
Baada ya kuondolewa na Magufuli, Januari Makamba na Nape Nnauye walionekana kuwa wamefifia kisiasa. Hata hivyo, baada ya kifo cha Rais Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua madaraka, Januari na Nape walirejeshwa kwenye baraza la mawaziri. Uteuzi wao ulionekana kama hatua ya kuwarejesha viongozi waliokuwa wamepoteza nafasi zao kwa sababu ya migogoro na Magufuli.
Urejeshaji huu ulikuwa na maana kubwa kisiasa, kwani ulionyesha kwamba Rais Samia alikuwa tayari kuwapa nafasi tena viongozi waliokuwa wamepoteza nafasi zao kwa sababu ya tofauti zao na mtangulizi wake.
Lakini Ghafla Leo Hii Wameondolewa Tena kwa Pamoja
Wanasema hakuna msomi au mtaalamu aliyeshiba pasi na kuangalia wengine wamesema nini? Tunadhani ni ipi sababu hasa ya kuondolewa kwa Januari Makamba kwa sababu tukimzungumzia Nape Nnauye tunaweza kusema moja kwa moja bila kupepesa macho unaweza hisi sababu ni kauli yake. Nape alisema kwamba matokeo ya uchaguzi hayapaswi kutokana na masanduku ya kura pekee, kauli ambayo ilizua mjadala mkali mtandaoni na ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kauli hii ilionekana kuwa na athari mbaya kwa chama na serikali, ikiwapa nafasi wapinzani kudai ushahidi wa udanganyifu wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa kisiasa, kauli za Nape zinaweza kuwa sababu kuu ya kuondolewa kwake, huku baadhi wakiona kuwa Rais Samia anatekeleza falsafa yake ya 4R (Reform, Rebranding, Realignment, and Reinvestment) kwa kuhakikisha viongozi wake wanakidhi viwango vya juu vya uadilifu na uwajibikaji.
Sababu ya Kuondolewa Januari ni Ipi?
Kwa mujibu wa Deus Kibamba, mhadhiri katika Kituo cha Kimataifa cha Mahusiano ya Kimataifa cha Dr. Salim Ahmed Salim, anasema wizara hii ni ngumu sio tu kwa Tanzania bali pia kwa nchi nyingine. Hii ni kutokana na umuhimu wake katika kuratibu safari za nje za viongozi wa serikali na mahusiano ya kimataifa kwa ujumla.
Kibamba aliongeza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wanatakiwa kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia kufanya mikutano na mazungumzo ya kimataifa bila kusafiri mara kwa mara, na kwamba changamoto nyingine ni kuhakikisha wizara hiyo inafanya kazi kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa taifa. Kibamba anabainisha kwamba mawaziri wa nje wanapaswa kuwa na uwezo wa kutafuta masuluhisho ya ndani kupitia teknolojia na kuwa na mipango madhubuti ya kuvutia uwekezaji kutoka nje badala ya kuwa tegemezi kwa mikopo.
Dr. Revocatus Kabobe, mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), alibainisha kuwa Rais Samia huenda hajapata mtu sahihi wa kuiongoza wizara hiyo na kwamba mawaziri walioteuliwa hawajafanikiwa kutafsiri vyema maono yake.
Kwa kuwanukuu wataalamu na wakongwe kwenye chambuzi za kisiasa, moja kwa moja wanaonyesha kuwa Januari Makamba hakuwa anatoshea katika kiti cha Wizara ya Mambo ya Nje. Lakini kwa upande wangu kama kijana chipukizi na Barobaro mwenye mitazamo ya nje kimataifa kama Wizara yenyewe ilivyo, naomba tuangazie zaidi katika suala la Umoja wa Afrika (AU).
RAIS SAMIA, JANUARI MAKAMBA NA FAUSTINE NDUGULILE - AU
Katika hatua ya kutambua mchango wake mkubwa katika sekta ya afya, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa baraka zake kwa Dkt. Faustine Ndugulile kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Uteuzi huu unaashiria nia ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika uongozi wa kimataifa wa afya na kuleta mageuzi muhimu katika bara la Afrika kupitia WHO.
Mara baada ya uteuzi wa Dkt. Ndugulile, Waziri wa Mambo ya Nje, Januari Makamba, alianza kampeni ya kumpigia debe kwenye vikao vya kimataifa.
Katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika uliofanyika Accra, Ghana, Januari Makamba alishiriki katika majadiliano na mawaziri wa mambo ya nje wa Zimbabwe, Lesotho, na Burundi, akiwashawishi kupigia kura Tanzania. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Januari aliandika:
"Nipo Accra, Ghana, kwa ajili ya
mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika ambapo tutajadili ajenda muhimu kwa
mustakabali wa Umoja wetu. Pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe,
Lesotho, na Burundi tukitafuta kura kwa ajili ya Dkt. Faustine, mgombea wetu wa
nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO."
Taarifa hii ilipokelewa vyema na wananchi na viongozi mbalimbali wa Afrika, ambapo pongezi nyingi kutoka kwa Wakenya zilionyesha kumkubali Januari kama kiongozi mwenye uwezo wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC).
WAGOMBEA NAFASI YA UENYEKITI AUC
Nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa sasa inawaniwa na wagombea watatu wakuu: Raila Odinga kutoka Kenya, Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibouti, na Fawzia Adam kutoka Somalia.
1. Raila Odinga, kiongozi wa upinzani nchini Kenya, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi hii. Raila ameanza kampeni za kushawishi mataifa 55 wanachama wa Umoja wa Afrika ili kupata uungwaji mkono wao.
2. Mahmoud Ali Youssouf, waziri wa mambo ya nje wa Djibouti, pia ametangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo. Djibouti inamsisitiza Youssouf kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika diplomasia.
3. Fawzia Adam, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Somalia, ni mgombea wa tatu katika kinyang'anyiro hiki. Somalia imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika kuendelea na kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Wagombea hawa watatu wanategemea uungwaji mkono kutoka kwa nchi zao na kanda mbalimbali za Afrika ili kuweza kupata nafasi hii muhimu.
Awali ilionekana kwamba Tanzania iliridhishwa na Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa AUC. Hata hivyo, majibu ya Wakenya wengi kwenye machapisho ya Januari Makamba yalionyesha kuwa wamechoshwa na wazee na wanahitaji damu changa. Wakati huo huo, kutokana na machafuko nchini Kenya, wengi wanaona kuwa mtu anayefaa kusaidia kukwamua hali hiyo ni kutoka nje, kwani mgombea wa ndani anaweza kuendeleza mitafaruku na machafuko
Hivyo, nikaona kuwa Januari Makamba huenda ameonyesha nia ya kugombea nafasi hiyo ya uenyekiti wa AUC jambo ambalo hadi mwisho wa makala hii sijalithibitisha hivyo kama unadhani kunasehemu nimethibitisha hivyo ni heri uache kusoma mapemaaaaa.
Kampeni za Dkt. Faustine Ndugulile zilikuwa na changamoto nyingi. Katika taarifa za mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kama The Eastleigh Voice, ilibainika kwamba Januari Makamba alikuwa akitajwa kama tishio kwa nafasi ya Raila Odinga kugombea uenyekiti wa AUC. Wakati huo huo, uvumi ulienea kwamba Tanzania ilikuwa ikipima uwezekano wa kumteua Makamba kwa nafasi hiyo.
Hata hivyo, Januari alisisitiza umuhimu wa umoja wa Afrika na malengo ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi nyingine za Afrika Mashariki kuhakikisha mgombea bora anapatikana kwa ajili ya AUC. Akizungumza kuhusu mkutano wa Accra, Januari alisema:
"Tanzania inazingatia umoja wa Afrika Mashariki na tutaamua kwa pamoja juu ya mgombea bora kwa uenyekiti wa AUC kupitia makubaliano ya nchi wanachama."
Mapendekezo na Mwisho wa Safari
Mapendekezo ya kumteua Januari kwa nafasi ya Mwenyekiti wa AUC yalipokelewa na vikundi mbalimbali vya viongozi vijana wa Afrika kama Tutu Leadership Fellows na African Young Global Leaders wa World Economic Forum. Waliandika barua kwa Rais Samia Suluhu, wakisisitiza sifa za Januari kama kiongozi mwenye mtazamo wa kiubunifu na mwenye nguvu, zinazohitajika kuleta mageuzi ndani ya AUC.
Katika barua hiyo, waliainisha hoja kuu tatu:
- Imani katika umoja wa Waafrika kama chanzo cha nguvu.
- Umuhimu wa Umoja wa Afrika kama chombo cha kuendeleza umoja huo na kuleta fahari kwa Waafrika.
- Uhitaji wa uongozi sahihi wa bara la Afrika ili kufanikisha umoja na ustawi wa Waafrika.
KUONDOLEWA KWA JANUARI MAKAMBA KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE
Mwisho wa safari hii ulikuja baada ya Rais Samia Suluhu rasmi kumtoa Januari Makamba kutoka kwenye baraza lake la mawaziri. Kwa kitendo hiki, ninaamini alidhamiria kumweka huru Makamba ili aweze kushiriki kikamilifu katika kampeni za kugombea uenyekiti wa AUC. Kupitia mitandao ya kijamii, hatua hii imepokelewa kwa hisia mseto; baadhi ya watu wakionyesha matumaini makubwa, huku wengine wakitoa tahadhari kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza.
Mabadiliko haya yana athari kubwa kwa mustakabali wa diplomasia ya Tanzania. Kuondolewa kwa Januari Makamba kunaweza kuwa na lengo la kumwandaa kwa nafasi kubwa zaidi katika siasa za kimataifa, huku Rais Samia akijaribu kupata mtu anayefaa zaidi kuendana na kasi yake katika wizara hiyo nyeti.
Aidha, uteuzi wa Dkt. Faustine Ndugulile kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO na kampeni za Januari Makamba kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika zinaashiria nia ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika uongozi wa kimataifa na kuleta mageuzi muhimu katika bara la Afrika. Ni hatua muhimu inayoweza kubadilisha taswira ya nchi na bara zima katika nyanja za afya na uongozi.
· Japo mpaka sasa haijafahamika je kuondolewa kwa Januari Makamba kumelenga kumuacha ajiandae kuwania kiti cha Mwenyekiti wa AUC
· Je kuondoka kwake/kwao kumesababishwa na migongano ya kisiasa kama ilivyokuwa kwa awamu ya Rais Magufuli
· Je kuondoka kwake/kwao ni moja ya njama za kisiasa na kuwaacha vijana hawa makini kuwa huru katika kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2025
- Je,
Januari Makamba katika nyanja za kimataifa amefanya maamuzi pasi na
ushirikiano mzuri na viongozi wake wa juu? Kwamaana mwanzo Tanzania
ilidhaniwa itamuunga mkono Odinga na je wazo la kugombea nafasi ya
uenyekiti wa AUC ni la kwake Januari pekeake au ni wazo la nchi (serikali)
· Au kuondolewa kwao kumetokana na utendaji mbovu hivyo Rais Samia ameamua kuzichanga upya karata zake na kuwapata watu anaodhani atafika nao katika njia aliyoidhamiria????
MWISHO
0 Comments