MFULULIZO WA MATUKIO MUHIMU MPAKA KIFO CHA RAIS JOHN KENNEDY









ALHAMISI, NOVEMBA 21

Rais John Kennedy na mkewe Jackie Kennedy wanawasili na Airforce One jimboni Texas katika uwanja wa ndege wa Carswell, katika viunga vya Fort Worth.
Rais na mkewe walikuwa wanatokea Santo Antonio, Huston ambako mchana Kennedy alihutubia katika chuo cha matabibu ya Jeshi la Anga kwenye kituo cha Brooks Airforce Base na Jioni yake alitoa hotuba katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Rice Hotel ambapo kulikuwa na kumbukumbu ya kifo cha Mbunge mshuhuri wa bunge la Congress aliyeitwa Albert Thomas.

Siku hii ya alhamisi Rais Kennedy na mkewe waliwasili Texas majira ya saa 5 na dakika 7 usiku na kupokelewa uwanja wa ndege na Raymond Buck rais wa Fort Worth Chamber of Commerce.



Pia katika ndege nyingine iliyombeba makamu wa Rais Lyndon B. Johnson walikuwa amefuatana na Gavana wa Jimbo la Texas, John Connally pamoja na hasimu wake mkubwa Seneta Ralph Yarborough.


Msafara wa Rais uliondoka uwanja wa ndege kupitia West Freeway ambapo licha ya kuwa ni muda wa usiku sana na mvua ilikuwa inanyesha, wananchi wengi walijitokeza na kujipanga barabarani kumpingia mikono.

Walifika Hotel Texas majira ya saa 5 na dakika 34 usiku, ambako katika hoteli hii ndipo ambapo Rais Kennedy na mkewe walilala kwa usiku huo.




IJUMAA, NOVEMBA 22


Siku hii ya Ijumaa ilianza mapema sana kwa Rais Kennedy kwa shughuli muhimu asubuhi na mapema.

Saa 2 na dakika 45 asubuhi, Rais Kennedy akiwa amefuatana na Makamu wa Rais Lyndon B. Johnson, pamoja na Mbunge wa Congress Jim Wright pamoja na Seneta Yarborough alikuwa anaongea na wananchi eneo la Eighth Street na katika hotuba yake hiyo aliimwagia sifa sekta ya usafirishaji wa anga ya jimbo la Texas.


Baadae majira ya saa 3 na dakika 10 Rais Kennedy alikuwa amesharejea hotelini kwake na alikuwa anatoa hotuba kwa wageni maalumu waalikwa katika ukumbi wa Hoteli.
Mkewe Jackie alichelewa na kuwasili dakika 15 baadae akipokelewa kwa makofi ya kishindo kutoka kwa wageni waalikwa.



Baada ya Rais Kennedy kumaliza hotuba yake fupi, swahiba wake mkubwa Kenny O'Donnell ambaye pia alikuwa ni katibu wa teuzi za Rais, alimfuata Roy Kellerman Afisa kiongozi wa Secret Services juu ya Safari ya Rais (Secret Service In charge).
Maagizo haya ambayo O'Donnell alimpa Agen Kellerman, ni kwamba alikuwa anamtaka awasiliane na Maafisa wenzake walioko Dallas ambako Kennedy alikuwa anaelekea na kuwataarifu kuwa kama hakukuwa na mvua basi anataka gari itakayombeba Rais iondolewe paa juu (liwe wazi) ili kumpa rais fursa ya kuonekana vyema na wananchi na kupungiana mikono.


Msafara wa Rais Kennedy uliondoka Hotel Texas majira ya kama saa 5 na dakika 10 asubuhi na majira ya saa 5 na dakika 23 Airforce One iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Carswell kwenye viunga vya Fort Worth na kuelekea Dallas.


Airforce One ilitua Dallas kwenye uwanja wa Love Field majira ya saa 5 na dakika 38.


Makamu wa Rais Johnson na Gavana Connally wao walikuwa wamewasili kabla ya Rais Kennedy, kwahiyo Airforce One ilipotua na kumshusha Rais na mkewe walilakiwa na Makamu wa Rais na Gavana wa Texas.


Msafara wa Rais Kennedy, Mkewe Jackie Kennedy, Makamu wa Rais, Gavana Connally na Seneta Yarborough uliondoka uwanja wa ndege wa Love Field majira ya saa 5 na dakika 55 asubuhi.


Msafara ulikiwa unatarajiwa kupitia katikati ya mji wa Dallas na kuwasili Dallas Business and Trade Mart majira ya saa 6 na dakika 15 mchana.


Msafara ulishika njia kuingia kati kati ya mji majira ya saa 5 na dakika 59…. Pasipo kujua, zilikuwa zimebaki dakika 31 tu za maisha ya Rais JF Kennedy.





SEHEMU YA PILI




Katika sehemu ya kwanza nilieleza kwa ufupi namna ambavyo Rais Kennedy, Mkewe Jackie na Makamu wa Ras Johnson walivyowasili Texas na kuanza safari yao ya kutoka uwanja wa ndege wa Love Field kuelekea Dallas Trade Mart kwa ajili ya chakula cha mchana na wanyeji wao.


Katika sehemu hiyo ya kwanza nilieleza msafara ulipofikia mpaka dakika 31 kabla ya kifo cha Rais Kennedy.



Tuendelee…


[​IMG]
RUTI AMBAYO MSAFARA WA RAIS KENNEDY ULIPITA BAADA YA KUINGIA DALLAS




DOWNTOWN DALLAS


Msafara wa Rais ulipokamata barabara kuingia katikati ya mji wa Dallas kuelekea Trade Mart ulikuwa kwenye mpangilio ufuatao;


- Gari ya Mbele

Gari ya mbele kabisa iliyokuwa inaongoza msafara ilikuwa ni gari aina ya Frord Mercury sedan.
Aliyekuwa anaendesha gari hii alikuwa ni mkuu wa Idara ya polisi katika mji wa Dallas ambaye aliitwa, Jesse Curry.
Katika siti ya mbele ya mkono wa kulia alikuwa ameketi Afisa wa Secret Services, Special Agent Winston.
Siti ya nyuma ya gari hii mkono wa kushoto alikuwa ameketi Bill Decker, Sheriff wa mji wa Dallas na siti ya mkono wake wa kulia alikuwa ameketi afisa mwingine wa Secret Services, SAIC Forrest Sorrels (SAIC - Special Agent In Charge).



- Gari ya Rais

Gari hii ambayo Rais Kennedy alipanda ilikuwa ni aina ya Lincoln Continental Convertible ya mwaka 1961, ambayo imeboreshwa ili kukidhi masuala ya kiusalama naendeshwa na afisa wa Secret Services, Agent William Greer. Pembeni yake katika siti ya mbele alikuwa ameketi afisa mwingine wa Secret Services, ASAIC Roy Kellerman (ASAIC - Assistant Special Agent In Charge), huyu ndiyo yule afisa ambaye alipewa maagizo na O'Donnel swahiba wa Kennedy na katibu wake anayeshughulika na masuala ya Teuzi, kuwa kama hakutakuwa na mvua mjini Dallas basi ahakikishe kuwa gari atakayopanda Rais inakuwa wazi bila paa la juu ili kuwarahisishia wananchi kumuona Rais kwa uzuri na kupungiana mikono.

Siti ya nyuma (kati za kati kati) mkono wa kulia alikuwa amekaa Gavana Connally huku mkono wake wa kushoto akiwa amekaa mkewe Nellie Connally.

Siti za nyuma kabisa za gari hii ya wazi, mkono wa kulia alikuwa ameketi Rais Kennedy huku mkono wake wa kushoto akiwa ameketi mkewe Jacqueline Kennedy.


Pembezoni/ubavuni mwa gari ambalo alikuwa amepanda Rais Kennedy, kulikuwa na pikipiki mbili za Polisi kila upande, ambapo mkono wa kushoto kulikuwa na piki piki zilizoendeshwa na Polisi wa kituo cha mji wa Dallas, ofisa Billy Joe Martin na ofisa Bobby Hargis.

Upande wa kulia kulikuwa na pikipiki zilizoendeshwa na ofisa James M. Cheney na ofisa Douglas L. Jackson.



- Gari ya nyuma ya Rais (follow up car)

Nyuma ya gari aliyopanda Rais Kennedy kulikuwa na gari aina ya Cadillac Touring Convertible ambayo iliwabeba maafisa wa Secret Services kwa ajili ya ulinzi wa Rais na First Lady.

Dereva wa gari hili alikuwa ni Agen Sana Kinney. Pembeni yake siti ya mbele kulia aliketi ATSAIC Emory Roberts (Assistant To Special Agent In Charge).

Katika mlango wa mbele mkono wa kushoto, kwenye mlango alikuwa ananing'inia Special Agent Clint Hill, ambaye anahusika na ulinzi wa First Lady.
Kwenye mlango mwingine wa mbele kulia alikuwa ananing'inia Special Agent Jack Ready.


Mlango wa nyuma kulia alikuwa ananing'inia Special Agent Paul Landis huku mlango wa mkono wa kushoto alikuwa ananing'inia Special Agent William T. McIntyre.

Ndani ya gari siti ya nyuma walikuwa wameketi watu wanne. Kulikuwa na Kenneth O'Donnell msaidi wa rais na katibu wake wa masuala ya teuzi, pia kulikuwa na David Powers ambaye naye ni msaidizi wa Rais na pambeni yao hawa mkono wa kulia aliketi Special Agent Glen Bennet na mkono wa kushoto aliketi Agent George Hickey.


- Gari ya makamu wa Rais


Nyuma ya gari iliyowabeba maafisa usalama wa ulinzi wa Rais ilifuata gari iliyombeba makamu wa Rais Lyndon B. Johnson.


Gari hii aina ya Lincoln Convertible ilikuwa inaendeshwa na Hurchel Jacks, afisa wa Polisi wa kituo kikuu cha Dallas. Pembeni yake mkono wa kulia alikuwa ameketi ASAIC Rufus Youngblood (Assistant Special Agent In Charge).
Siti ya nyuma walikuwa wamekaa Seneta Ralph Yarborough (kushoto), Lady Bird Johnson (kati kati) na kulia alikuwa ameketi Makamu wa Rais Lyndon B. Johnson.



Nyuma ya gari iliyombeba makamu wa Rais kulikuwa na gari ya maafisa wa Secret Service maalumu kwa ajili ya ulinzi wa Makamu wa Rais Lyndon B. Johnson (VP followup car).


Nyuma ya VP followup Car kulikuwa na gari ya Mayor wa Dallas, iliyombeba Mayor Earle Cabell na mkewe Elizabeth Cabell.


Nyuma yao kulikuwa na gari iliyowabeba waandishi wa habari kutoka vituo vikuvwa vya kitaifa (National Press Pool).


Nyuma ya gari hii zilifuata gari nyingine tatu za watu wa Picha (Camera Cars), ambazo zilibeba wapiga Picha za video, picha za mnato na waandishi wa habari wenyeji wanaofanyia kazi vyombo vya habari jimboni Texas.


Nyuma ya gari hii tatu kulikuwa na gari nyingine tatu zilizowabeba wabunge wote wa Congress kutoka jimbo la Texas.


Na mwishoni kabisa mwa msafari kulikuwa na magari makubwa mawili (Buses) ambazo zilibeba watumishi wengine wa Rais wa ngazi za chini.
Mfano waandishi wa habari wa Ikulu, makatibu wa Idara za Ikulu, Daktari wa Rais na kadhalika.


Kisha nyuma ya mabasi haya mawili msafara ulimaliziwa na gari ya Polisi iliyofuatia nyuma.




Hii ndio picha kamili ya msafara wa Rais Kennedy ulipoyoka uwanja wa ndege wa Love Field kuelekea Trade Mart kati kati ya mji wa Dallas.

Kama nilivyosema awali kwamba, umbali kati ya uwanja wa ndege wa Love Field na alikokuwa anaelekea Kennedy (Trade Mart) ni kilomita 16 tu, lakini zilipangwa msafara usafiri kwa mwendo wa taratibu na kutumia dakika 45 ili kumpa Rais muda wa kutosha kusalimiana na wananchi njiani.


Wananchi walikuwa wamejitokeza wengi haswa na kujipanga barabarani kumlaki Rais.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu laki moja na nusu mpaka laki mbili walikuwa wamejitokeza.


Msafara ulizidi kuchelewa zaidi baada ya Rais Kennedy kuamuru msafara kusimama mara mbili barabarani nje ya ratiba iligopangwa ili aweze kiwapa mikono wananchi.

Mara ya kwanza aliamuru msafara usimame ili kuwapa mikono watawa wa kikatoliki waliokuwa wanampungia mikono barabarani. Mara ya pili walikuwa ni wanafunzi wa shule ambao nao walikuwa wamejipanga barabarani kumshangilia.



Majira ya saa 6 na dakika 29 msafara wa Rais uliingia katika eneo kubwa (mtaa) ujulikanao kama Dealey Plaza ambao zamani ulikuwa na bustani na maeneo ya watu kupumzika.

Mbele yao ya macho lilikuwa linaonekana "jengo lililobeba kifo" cha Rais Kennedy, Jengo la Texas School Books Depository.


Wakiwa bado eneo hili hili la Dealey Plaza, msafara wa Rais ukakata tena kona ndogo kutoka mtaa mdogo wa Houston Street na kuingia mtaa wa Elm Street.


Bado jengo la Texas School Book Depository, "jengo lililobeba kifo" cha Kennedy lilikuwa katika upeo wa macho yao japokuwa walikuwa wanaelekea kulipita.


Kennedy na Mkewe Jackie walikuwa wanapungia mikono mamia ya wananchi waliojipnga barabarani kumshangilia.

Kwa kuzingatia kuwa Kennedy alipata kura kiduchu eneo hili la Dallas wakati wa uchaguzi mkuu, hivyo mkewe Jackie akamgeukia na kumtania.

"…kwa hizi shamra shamra, huwezi kusema eti wananchi wa Dallas wanakuchukia…" Jackie akaongea huku anatabasamu kumuangalia mumewe.


"…hakika! Siwezi kusema wananichukia.!!"

Kennedy akamjibu kwa kifupi mkewe huku anatabasamu na kuwapungia mikono wananchi.

Na hii ndio ilikuwa kauli ya mwisho ya Rais JF Kennedy… tayari ilikuwa ni saa 6 na 30. Na mbele yake alikuwa amebakiza chini ya sekunde 15 za uhai wake.




SEHEMU YA TATU



Katika sehemu ya Pili nilieleza namna msafara wa Rais Kennedy ulivyopangiliwa kutoka uwanja wa ndege kuelekea Trade Mark na kwasili kwao mtaa wa Elm Street na nikamaliza sehemu ile ya pili muda wa sekunde 15 kabla ya kifo cha Kennedy.



Tuendelee…




Mlio wa kwanza wa risasi wengine wanadai kwamba hawakuusikia, na hata baadhi ya maafisa wa Secret Services baadhi yao nao wanadai kwamba hawakuusikia. Na hata wale waliosikia walidai kwamba walidhani labda ilikuwa ni pancha ya tairi la gari au kitu kingine, hii ndio sababu ukiangalia katika kipande cha video (Tazama chini) baada ya kupigwa kwa risasi ya kwanza hakukuwa na taharuki yoyote kutoka kwa wanausalama wa kumlinda rais na msafara uliendelea kama kawaida.


Risasi hii ilipigwa katika muda ambao Rais Kennedy, mkewe Jackie na Gavana Connally wote walikuwa wameguukia mkono wa kushoto kupungia wananchi na ghafla wote wakageuka mkono wa kulia kupungia wananchi walio upande huo.

Ni muhimu kukumbuka kwamba katika muda huu walikuwa wekwisha lipita Jengo la Texas School Book depository, na wamelipa mgongo kwa kuliacha umbali wa takribani mita 81.


Risasi ya pili kupigwa (risasi ya kwanza nitaiongelea baadae) ilifyatuliwa sekunde ambayo Kennedy ameinua mkono mmoja juu akiwaoungia wananchi.


Risasi hii ilimpenya nyuma yake katikati kabisa ya shingo na nyama ya juu ya bega na kusababisha uharibu Mdogo kwenye uti wa mgongo, na kisha kupenya ndani na kuharibu sehemu ya juu kabisa ya pafu la kulia na kutokea kooni ikiharibu sehemu kubwa ya koromeo.

Baada ya kupigwa na risasi hii, katika kipande cha video unaweza kumuona Rais Kennedy akiwa amekunja ngumi na kuelekeza mkono mbele ya uso wake usawa wa mdomo kama vile anakohoa na kuinama kwa mbele kidogo akiengemea upande wa kushoto aliko mkewe.

Pia unaweza kumuona mkewe akiwa anamkumbatia kwa kuzungusha mkono wake mabegani kwa Kennedy kumuuliza kama yuko 'OK'! (Mpaka muda huu hakujua kama mumewe amepigwa risasi).


Risasi hii hii ya pili iliyompiga Kennedy, ilipotoka kooni kwa Kennedy ilienda moja kwa moja ya kumpiga Gavana Connally!
Risasi hii ilimpiga Gavana Connally mgongoni chini kidogo ya kwapa upande wa kulia na kutengeneza tundu la umbo la duara na kuharibu kiasi cha inch 4 cha mbavu yake ya tano upande wa kulia na kisha kutokea kifuani katika chuchu.

Risasi hii hii baada ya kutoka kifuani kwa Gavana Connally kupitia kwenye chuchu ilitua kwenye mkono wa kulia wa Gavana Connally, juu kidogo ya kiganja na kuvunja vunja sehemu hiyo katika vipande vinane.

Risasi hii hii, hatimaye ikatua kwenye paja la kushoto la Gavana Connally.


(Nitaeleza huko mbeleni kuhusu utata wa risasi hii ya pili iliyompata Kennedy na Gavana Connally kwa pamoja na ile Risasi ya kwanza ambayo haikuleta madhara yoyote).


Risasi ya pili kumpata rais (ambayo ilikuwa ni risasi ya tatu kupigwa) ilimpata kichwani upande wa juu kulia.

Risasi hii ilifumua kabisa eneo hilo la kichwa na kusababisha sehemu ya ubongo wa mbele kumwagika.

Damu nyingine ikaruka nyuma ya gari kwenye 'trunk' na nyingine kutua mpaka kwenye mkono wa kushoto wa afisa wa Secret Services aliyekuwa anaendesha gari ya wanausalama waliokuwa gari ya nyuma ya Rais.


Ndani ya sekunde mbili baada ya mumewe kufumuliwa na risasi kichwani, First Lady Jacqueline Kennedy akaruka kutoka kwenye siti yake na kuanza kuparamia nyuma ya gari kwenye trunk.
Tofauti na wengi wanavyodhani kwamba alikuwa anajaribu kukimbia kuokoa maisha yake, ila ukweli ni kwamba alikuwa anaokota kipande cha mfupa wa fuvu la kichwa kilichodondoka kwenye nyuma ya gari kwenye trunk baada ya mumewe kufumuliwa kichwa na risasi. Baada ya kukichukua haraka haraka akarejea kwenye siti yake. (Tazama tena kipande cha video nilichokiweka kwa makini).


Sekunde hii hii ambayo First Lady alikuwa anaparamia gari kwenye trunk, katika gari ya nyuma (follow up car), Special Agent Clint Hill ambaye alikuwa ananing'inia kwenye mlango wa mbele kushoto akaruka na kuanza kuikimbilia gari iliyombeba rais na first lady.
Dereva wa gari la rais alikuwa ameongeza mwendo baada ya mushkeli kutokea na dhahiri kuonekana kwamba rais yuko hatarini.
Hivyo basi ilimbidi Clint Hill kujaribu kuparamia gari mara kadhaa mpaka alipofanikiwa kuidandia gari na mara moja kuwafunika rais na first lady akiwakinga kwa kutukia mwili wake kama ngao.


Baada ya Agent Clint Hill kuwakinga Rais na mkewe dhidi ya shambulio lingine lolote la risasi kuwafikia, gari ya rais liliendeshwa kwa kasi kubwa likifuatiwa na pikipiki za pembeni na ile follow up car ya maafisa usalama.


Wakati haya yote yanatokea zilikuwa zimebaki takribani dakika tano pekee kufika walikokuwa wanaelekea, Trade Mart.
Kwahiyo baada ya gari iliyombeba rais kuanza kuendeshwa kwa kasi, takribani saa 6 na dakika 35 walipita eneo la Trade Mart na kuelekea moja kwa moja hospitali ya Parkland Memorial Hospital ambako waliwasili majira ya saa 6 na dakika 38 na kupokelewa kisha Rais Kennedy alipelekwa moja kwa moja chumba cha dharura.


Licha ya watu wa usalama kujitahidi sana kuratibu taaarifa za kilichotokea zisivuje kabla ya taarifa rasmi ya serikali, lakini majira ya saa 6 na dakika 40 kituo cha televisheni cha CBS kikakatisha Igizo lililokuwa linaonyeshwa kwenye televisheni yao na kutoa "Breaking News" kuwa msafara wa Rais umeshambuliwa huko Dallas.


Baadae kama muda wa saa 6 na dakika 45, Dan Rather mwandishi wa habari wa kituo cha CBS alifanya mawasiliano kwa siri sana na daktari anayemfahamu hapo hospitalini na kuvujishiwa taarifa kuwa kuna uwezekano mkubwa Rais Kennedy hayuko hai.

Ifahamike kwamba maafisa wa Secret Services waliwaleta hapa viongozi wengine wote wakuu waliopo kwenye msafara, yaani First Lady Jacqueline Kennedy, Makamu wa Rais Johnson, Mkewe Lady Bird na Gavana Connally ambaye alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi.


Ilipofika saa 7 kamili madaktari wakatoa taarifa yao kwa viongozi wa serikali na wanausalama waliokuwepo hapo kwamba, licha ya kutumia ujuzi wao wote na maarifa yao yote, wameshindwa kuokoa maisha ya Rais JF Kennedy, kwamba Rais Kennedy amefariki.!!


Huko mtaani habari zilikuwa zinaenea kwa kasi kama moto wa kifuu, kuwa Rais Kennedy amefariki, hivyo kwa busara watu wa usalama wakashauri kuwa itolewe taarifa rasmi kuhusu kifo cha Rais Kennedy ili kuepusha mkanganyiko na taharuki iliyopo mtaani.

Makamu wa Rais Johnson akakubali hilo lakini akaamuru taarifa hiyo itolewe kwa umma mara baada ya yeye kuondoka hapo hospitali kwa usababu ya usalama wake, kwamba hataki yeyote ajue kuwa yuko hapo hospitali kwa kuwa kwa vile Rais ameuwawa tayari yawezekana yeye kama Makamu wa Rais akawa ni "next target"!


Saa 7 na dakika 26 Makamu wa Rais Lyndon B. Johnson akaondolewa kwa siri kubwa kutoka Parkland Memorial Hospital na kupelekwa uwanja wa ndege wa Love Field ambako Airforce One ilikuwa imepaki.



Baada ya Makamu wa Rais kuondoka tu, dakika saba baadae yaani saa 7 na dakika 33 Katibu Msaidizi wa Mawasiliano Ikulu Bw. Malcolm Kilduff ya Marekani akafanya mkutano na waandishi wa habari hapo hapo hospitali na kuutangazia rasmi ulimwengu kuwa Rais JF Kennedy amefariki baada ya kudunguliwa na risasi na mtu asiyejulikana.
Bw. Kilduff hakujibu swali lolote la waandishi wala kutoa taarifa nyingine yoyote. Alipotoa taarifa hii tu akaumaliza mkutano na wanahabari.


Baada ya waandishi wote kuondoka na kubakia watu wa serikali pekee na wanausalama ndani ya Hospitali kulitokea kisa ambacho naamini wengi hawajawahi kukisikia.


Ni kwamba, katika sheria za Marekani kipindi hicho zilikuwa zinaelekeza kwamba, endapo Rais atafariki akiwa jimbo Fulani.. Mwili wake unakuwa chini ya mamlaka ya jimbo na sio serikali kuu.

Sasa, yule bwana swahiba wa Rais Kennedy na Katibu wake wa teuzi Kenneth O'Donnell, yule ambaye alimuamuru Afisa wa Secret Services, Agent Kellerman kuwa gari la Rais liondolewe paa na kubaki 'kibnda wazi', akatoa tena maelekezo kwa wanausalama wauondoe mwili wa Rais Kennedy kutoka hapo hospitalini na kuipeleka uwanja wa ndege wa Love Field na kuipakia katika Air Force One.


Lakini madaktari walikataa mwili huo kuondolewa hospitalini bila kufanyiwa 'Autopsy' (uchunguzi wa kina wa kidaktari kuhusu chanzo cha kifo) ukizibgatia kuwa Rais Kennedy amekufa kwa mauaji ya kukusidiwa.


Bw. Kenneth O'Donnell akasisitiza kuwa hakuna muda wa kutosha kufanya Autopsy kwani Air Force One inatakiwa iondoke mara moja kuwarudisha Makamu wa Rais na First Lady Washington kwa sababu za kiusalama na First Lady amekataa kuondoka bila mwili wa mumewe.

Madaktari wakashilia msimamo wao kuwa hawawezi kuuachia mwili wa Rais bila kufanyiwa Autopsy. Na kusisitiza wanalolisema wakatumia kifungu cha sheria nilichokitaja hapo juu kuwaeleza kuwa wao (Kenneth na wanausalama) kama watumishi wa serikali kuu hawana mamlaka juu ya mwili wa Rais bali wao (madaktari) kama watumishi wa jimbo la Texas ndio wenye mamlaka juu ya mwili wa Rais.

Mzozo ukawa mkubwa sana mpaka kufikia hatua Kenneth O'Donnell na wanausalama wakataka kuutoa mwili wa Rais Kennedy kwa kutumia nguvu.
Hii ikawalazimu madaktari kuita maafisa wa polisi (watumishi wa jimbo la Texas) kuwasaidia kuwadhibiti Kenneth na wanausalama wa Secret Services.

Madaktari wakatanda mlangoni pamoja na Maafisa wa polisi wakiwa wameshikilia bastola kuwanyooshea Kenneth O'Donnell na wanausalama wa Secret services kuwaamuru waache mwili wa Rais.
Upande wa pili nao Kenneth na wanausalama walikuwa nao wamechomoa bastola kuwanyooshea madaktari na polisi wa jimbo la Texas kuwa wapishe mlangoni.


Wakati mzozo huo unaendelea hospitali ya Parkland Memorial Hospital, huko uwanja wa ndege wa Love Field, ndani ya Air Force One Jaji wa mahakama Kuu, Sarah Hughes alikuwa anamuapisha Makamu wa Rais Lyndon B. Johnson kuwa Rais wa Marekani.

[​IMG]
MAKAMU WA RAIS LYNDON B. JOHNSON AKIAPISHWA NA JAJI SARAH HUGHES KUWA RAIS WA MAREKANI

Na huko mitaani wananchi walikuwa wako kwenye sintofahamu kubwa!! Ni nini kimetokea? Nani amemuua Rais? Amewezaje kutekeleza hilo? Sababu gani imemponza Kennedy kuuwawa??

Maswali yalikuwa mengi na magumu pasipo majibu ya dhahiri!!



SEHEMU YA NNE




Katika sehemu ilitopita nilijadili namna ambavyo msafara wa Rais Kennedy ulishambuliwa mpaka kupelekea kifo chake.

Katika sehemu hii ya nne nitajadili kuhusu muhusika/wahusika wa kifo chake.

Katika sehemu hii ya nne nitajadili kuhusu 'version' ya serikali kuhusu nani alimuua Kennedy na kwa lengo gani na baada ya hapo nitajadili kuhusu ushahidi unaoashiria dhahiri kwamba kuna kitu zaidi serikali wanakijua kuhusu wahusika halali wa kifo cha Kennedy lakini wanajaribu kuuficha ukweli.




Tuendelee…






UHUSIKA WA LEE HARVEY OSWALD

Baada ya kushambuliwa kwa msafara wa Raid Kennedy na hatimaye kupelekea kifo chake, mara moja ndani ya masaa mchache akakamatwa mtu anayejulikana kama Lee Harvey Oswald na kushutumiwa kuhusika na tukio hili.


Hii ilikiwaje? Nitaeleza kile ambacho serikali ya Marekani wanajaribu ulimwengu wote waamini…



Marion Baker ni afisa polisi wa eneo la Dallas na siku ya tukio alikuwa amepangiwa kuwa moja ya wasindikiza msafara kwa pikipiki.
Piki piki yake ya polisi ilipangwa nyuma ya magari waliyopanda waandishi wa habari kama ambavyo nilielezea mpangilio wa msafara katika sehemu ya pili ya makala hii.


Baker anaeleza kwamba siku hiyo ya tukio, akiwa kwenye msafara sekunde chache baada ya kukata kona kutoka Huston Street na kuingia Elm Street msafara ulipotembea umbali wa kati ya futi 60 au 80 alisikia mlio mkubwa wa risasi. Baker anadai kwamba kwa uzoefu wake aligundua kuwa mlio huo ni wa 'Rifle' yenye nguvu kubwa na kuzingatia mlio uliotoka alihisi kwamba bunduki hiyo imefyatuliwa kutoka eidha Jengo la mbele yake (Texas School Book Depository) au jengo lililo mkabala na jengo hili kwa upande wa kulia, yaani jengo la Dallas Textile Building (DalTex).


Baker anaeleza kwamba, alipoangalia kwa umakini zaidi katika jengo la Texas School Books Depository akaona njiwa waliokuwa juu ya jengo wanaruka na kutawanyika kutoka kwenye paa.

Baker anaeleza kwamba moja kwa moja akaendendesha pikipiki yake mpaka kwenye kona ya Huston Street na Elm Street ambako alipaki pikipiki yake na kisha kuelekea kwenye jengo la Texas School Books Depository na kuingia ndani ambako alikutana na msimamzi wa jengo hilo Bw. Roy Truly.

Moja kwa moja baada ya kumueleza kwa haraka haraka kuhusu kilichokuwa kinaendelea huko barabarani alikotoka na kwanini yuko hapa, yeye na Roy wakapanda mpaka ghorofa ya kwanza na kuanza kupiga kelele mtu yeyeto aliyepo juu ashushe lifti kuja chini.
Miaka hiyo lifti nyingi hazikuwa na mfumo kama huu wa sasa ambapo unabofya kitufe na lifti inakufuata ghorofa ulilopo. Kipindi hicho ilikuwa inabidi mtu aliyepo ghorofa ambalo ndipo lifti ilikuwepo kwa muda huo airuhusu kushuka chini au kwenda juu kulingana na uhitaji wa huo.

Baada ya Baker na Roy kuita kwa sekunde kadhaa bila majibu wakaamua watumie ngazi za kawaida za jengo kwenda juu.

Wakapanda mpaka ghorofa ya pili ambako wakiwa wanaelekea kupanda ngazi kwenda ghorofa ya juu zaidi, Baker anadai kwamba alisikia mjongeo kwenye chumba kilichopo karibu yao. Chumba hiki kilikuwa kinatumika kama chumba cha chakula na wafanyakazi kwenye jengo hili.

Baker akachomoa bastola yake kutoka kiunoni na kufungua chumba hiki. Ndani ya chumba hiki walimkuta Lee Oswald.
Wanaeleza kuwa Oswald hakuonekana kuwa mtu mwenye mashaka au 'kupaniki' ila tu alishtuka kuona Polisi amemmnyooshea bastola.
Inaelezwa kuwa Oswald alikuwa anaonyesha dalili zote za mtu ambaye hakuwa anajua ni nini kilikuwa kinaendelea.

Msimamizi wa jengo alimtambulisha Oswald kwa askari kuwa alikuwa ni mfanyakazi wa jengo hilo, hivyo ikambidi polisi amuache Oswald na kuendelea na upekuzi katika floor za juu.

Purukushani yote hii kutoka muda ambao Baker alisikia mlio wa risasi akiwa kwenye msafara wa Rais mpaka kuja kukutana na Oswald ghorofa ya pili ya jengo la Texas School Books Depository, ilichukua kama sekunde 74 mpaka sekunde 90 tu.


Kwa mujibu wa ripoti ya kamisheni maalumu iliyoundwa nanserikali ili kuchunguza kifo cha Rais Kennedy, The Warren Commission wanaeleza kwamba inakisiwa kuwa Oswald aliondoka kwenye jengo la Texas School Books Depository muda wa saa 6 na dakika 33 kupitia mlango wa mbele huku akiwa ameshika soda mkononi kwa mujibu wa ushahidi wa mwanamama ambaye alikuwa anafanya kazi kama secretary kwenye jengo hili.



Inaelezwa kwamba, baada ya upekuzi mnamo saa 6 na dakika 50, bunduki, Rifle aina ya Italian Carcano iligunduliwa ikiwa imefichwa kwenye lundo la vitabu katika ghorofa ya sita.

Baada ya kugundulikwa kwa bunduki hii mnamo majira ya saa 6 na dakika 50 jengo hili likawa 'sealed' kuzuia mtu yeyote asitoke au kuingia.

Lakini ajabu ni kwamba kule barabarani ambapo Rais Kennedy alidunguliwa, kulikuwa hakujawekwa kizuizi chochote kuzuia watu wasipite ili kuepusha kuharibu 'crime scene', na kuna rekodi za video zikionesha magari yakiendelea kupita barabarani kama kawaida eneo lile ambalo dakika chache kumetokea mauaji ya Rais.


Ripoti ya Warren Commission inaeleza kwamba mara baada ya Oswald kutoka kwenye jengo la Texas School Books Depository, Oswald alitembea kwa miguu umbali wa kupita majengo saba (seven blocks) na kisha kupanda bus.
Bus lilitembea kwa muda mchache kabla ya kukwama kwenye foleni ya barabarani. Baada ya bus alilopanda kukwama kwenye foleni, Oswald alishuka na kutembea kwa mguu mpaka kwenye kituo cha mafuta. Hapo alichukua taxi ambayo ilimbeba mpaka mtaani kwake lakini hakushukia nje ya nyumba yake, taxi ilienda kumshusha majengo kadhaa kupita nyumba yake. Baada ya kushuka kwenye Taxi akatembea kurudi nyuma mpaka nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa mfanyakazi wa usafi kwenye jengo ambalo Oswald alikuwa amepanga, Earlene Roberts, anasema kwamba Oswald aliwasili nyumbani kwake 1026 North Beckley Avenue majira ya saa 7 kamili mchana na hakukaa sana ndani kwani aliondoka tena kama dakika tatu au nne baada ya kuwasili.


Earlene anadai kuwa alimuona Oswald amesimama mbele ya nyumba akiwa anasubiri gari muda mchache baada ya kumuona amewasili hapo kabla.


Ilipofika majira ya saa 7 na dakika 15 mchana polisi walipokea taarifa juu ya kupigwa risasi kwa polisi mwenzao J.D Tippit katika makutano ya barabara za 10th St. na Patton Avenue. Sehemu hii ni takribani kilomita moja tu kutoka nyumbani kwa Oswald.


Bado kuna utata na ubishani mkubwa kwanini polisi walimuhusisha Oswald na kupigwa risasi kwa polisi J.D Tippit, lakini inaelezwa kwamba Oswald alionekana akitembea kwa miguu kuelekea jumba la maonyesho ya sinema la Texas Theatre.
Kuna bwana mmoja anaitwa Johhny Calvin Brewer ambaye alikuwa anafanya kazi katika duka la viatu liitwalo Hardy's shoes Store ambalo liko ghorofa moja na ilipo Texas Theatre anadai kwamba alimuona Oswald akijificha sura mara baada ya magari ya polisi kupita karibu yake huku yakiliza king'ora.

Bw. Brewer anadai kwamba akamfuatilia Oswald alikokuwa anaelekea na akamuona anaingia kimagendo bila kulipia mlangoni Texas Theatre muda ambao mkata tiketi Bi. Julie Postal alikuwa amejisahau na kuangalia pembeni.


Inaelezwa kwamba Brewer akamtaarifu bibie Julie kuhusu Oswald aliyeingia kimagendo ndani ya Theatre na baada ya hapo wakapiga simu polisi kuwafahamisha kuwa ndani ya Theatre kulikuwa na mtu ambaye walikuwa wana mashaka naye.


Ndani ya dakika chache, kufumba na kufumbua zilifika zaidi ya gari za polisi 24, pamoja na ma-sheriff na wapelelezi.

Baada ya lundo hili la wanausalama kuwasili, mnamo majira ya saa 7 na dakika 50 mchana Lee Harvey Oswald akakamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha polisi J.D Tippit na muda mchache baada ya kufikishwa kituo cha polisi, Oswald aliongezewa mashtaka na kuhusishwa pia na kumdungua kwa risasi na kumuua Rais JF Kennedy.!!

[​IMG]
LEE HARVEY OSWALD AKIKAMATWA KUTOKA TEXAS THEATRE 

[​IMG]
LEE OSWALD CHINI YA ULINZI MKALI WA WANAUSALAMA

Post a Comment

0 Comments