Sehhem ya 1:Nani aliyepanga haya mauaji ya hawa Marais Abraham Lincoln na John Kennedy?

Abraham Lincoln alichaguliwa kuingia katika Bunge la Marekani mwaka 1846. John F. Kennedy naye alichaguliwa kuingia katika Bunge hilo mwaka 1946. Hiyo ni tofauti ya miaka 100, au tuseme karne moja tangu kutokea kwa tukio moja hadi lingine. Pengine ni historia ilijirudia. Lakini kuna mengi zaidi ya hilo.

Mwaka 1856 Lincoln hakupata kura za kumtosha kupendekezwa kuwa mgombea Urais. Mwaka 1956 Kennedy naye alishindwa kuteuliwa kugombea umakamu wa Rais 1956. Hiyo ni miaka 100 barabara.

Abraham Lincoln alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1860. John Kennedy akachaguliwa kuwa Rais 1960. Katika mbio za uchaguzi, Lincoln alimshinda Stephen Douglas aliyezaliwa mwaka 1813. Kennedy naye alimshinda Richard Nixon aliyezaliwa 1913.

Wote wawili—Lincoln na Kennedy—walijishughulisha na haki za kiraia, na wote walisomea sheria. Wake zao—Mary Todd Lincoln na Jacqueline Bouvier Kennedy—walifiwa na watoto wakati waume zao wakiwa Ikulu. Mtoto wa Lincoln aliitwa Edward Baker Lincoln aliyefariki mwaka 1846 akiwa na umri wa miaka minme.

Mtoto wa Kennedy, Patrick Bouvier Kennedy, alifariki dunia mwaka 1963 katika muda wa saa 48 tangu alipozaliwa. Watoto wote hao walikuwa wakitumia majina ya koo za mama zao—Bouvier (Kennedy) na Baker (Lincoln).

Wote wawili, Abraham Lincoln na John Kennedy, waliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Ijumaa na walipigwa risasi kichwani. Tofauti ni idadi tu ya risasi zilizopigwa.

Katibu wa Abraham Lincoln aliitwa Kennedy, na katibu wa John Kennedy aliitwa Lincoln. Marais wote wawili waliuawa na watu waliotoka kusini mwa nchi hiyo, na wote, baada ya kuuawa, walirithiwa na watu waliotoka kusini mwa Marekani.

Marais wote wawili, Kennedy na Lincoln, walikuwa na Makamu wa Rais waliokuwa na majina ya ‘Johnson’. Makamu wa Rais wa Lincoln aliitwa Andrew Johnson ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi mwaka 1847. Makamu wa Rais wa Kennedy aliitwa Lyndon Johnson ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi mwaka 1947.

Warithi wao wote (Makamu wao wa Rais) waliitwa Johnson. Andrew Johnson, ambaye alimrithi Lincoln, alizaliwa mwaka 1808. Lyndon Johnson, aliyemrithi Kennedy, alizaliwa mwaka 1908.

John Wilkes Booth, ambaye ndiye muuaji wa Lincoln, alizaliwa mwaka 1838. (si mwaka 1839 kama ilivyodaiwa na masimulizi fulani ya historia). Lee Harvey Oswald, ambaye ‘alimuua’ Kennedy, alizaliwa mwaka 1939. Ni tofauti tu ya mwaka mmoja.

Wauaji wote wawili walijulikana kwa majina yao yote matatu, na majina yao kila mmoja yana herufi 15.

Lincoln alipigwa risasi akiwa katika ukumbi ulioitwa “Ford” kwa heshima ya aliyekuwa mtengenezaji maarufu wa magari duniani aliyeitwa Henry Ford. John Kennedy alipigwa risasi akiwa katika gari lililoitwa "Lincoln" lililotengenezwa na kampuni ya Ford Motor Company iliyomilikiwa na Henry Ford.

Muuaji Booth, baada ya kumuua Lincoln, alikimbia kutoka ukumbini alimofanya mauaji na akakamatiwa katika bohari. Tofauti kidogo na huyo, ‘muuaji’ Oswald alikimbia kutoka katika bohari na kukamatiwa ukumbini. Wauaji wote wawili, Booth na Oswald, waliuawa kabla kesi dhidi yao hazijaanza.

Rais Lincoln alizaliwa Februari 12, 1809 na kufariki Aprili 15, 1865 akiwa na umri wa miaka 56. Rais Kennedy alizaliwa Mei 29, 1917 na kufariki dunia Novemba 22, 1963 akiwa na umri wa miaka 46.

Mwezi mmoja kabla Lincoln hajauawa alikuwa katika eneo linalojulikana kama Monroe lililoko Maryland, Marekani. Kwa upande mwingine, mwezi mmoja kabla John Kennedy hajauawa alionekana akiwa na mchezaji sinema maarufu aliyeitwa Marilyn Monroe, ambaye waandishi wengine wanadai kuwa alikuwa hawara yake.

Sinema peke yake iliyokamilika ambayo inaonyesha mauaji ya John Kennedy ilitengenezwa na mtu aliyeitwa Abraham Zapruder, na maelezo yaliyokamilika yanayoelezea mauaji ya Abraham Lincoln yaliandikwa na mtu aliyeitwa John Zelfindorfer.

Mtoto wa Lincoln aliyeitwa Tad alizikwa Julai 16, 1871. Baadaye maiti ya mtoto huyo ilichimbuliwa kutoka katika kaburi alimozikwa na kupelekwa kuzikwa katika eneo lingine la makaburi.

Mtoto wa John Kennedy, JFK Jr., akirusha angani ndege yake, alitoweka bila kujulikana alikokuwa na hatimaye kukutwa amekufa pamoja na abiria wake wawili waliokuwa katika ndege hiyo. Mmoja wao alikuwa mchumba wake. JFK Jr., alifariki Julai 16, 1999 (tazama hizo tarehe). Baada ya kupatikana maiti yake ilichukuliwa na kuzikwa upya.

John Kennedy na Abraham Lincoln, wote, kwa nyakati tofauti, walisoma sheria na wote waliwahi kufanya kazi jeshini.

Kennedy alichaguliwa kuwa Rais Novemba 8. Lincoln alichaguliwa kuwa Rais Novemba 8. Kennedy alikuwa mtoto wa pili katika familia yake. Lincoln naye alikuwa mtoto wa pili katika familia yake.

Wote wawili walitumia majina ya babu zao. Kennedy alikuwa na watoto walioitwa Robert na Edward, kadhalika Lincoln alikuwa na watoto walioitwa Robert na Edward. Kennedy alizaa watoto wanne, na Lincoln alizaa watoto wanne.

Lincoln alikuwa na daktari wake aliyeitwa Charles Taft. Kennedy naye alikuwa na daktari wake aliyeitwa Charles Taft. Lincoln alikuwa na rafiki na mshauri aliyeitwa William Graham. John Kennedy alikuwa na rafiki na mshauri aliyeitwa Billy Graham. Inasemekana kuwa Billy na William ni majina mawili yanayotofautiana katika kuandikwa lakini si katika maana.

Chanzo kimoja cha habari kinasema kuwa mwaka mmoja kabla Lincoln hajauawa alipokea barua 80 zilizotishia maisha yake. Kadhalika, chanzo hicho hicho kinasema, mwaka mmoja kabla ya kuuawa Kennedy alipokea barua 800 za kutishia uhai wake. Barua za kennedy ni mara kumi ya zile za Lincoln, lakini namba yake ni nane.

Lincoln aliuawa mbele ya mkewe na Kennedy aliuawa mbele ya mkewe. Wake zao hawakudhurika wakati wa mauaji ya waume zao. Orodha hiyo inaweza kuendelea hadi tukajaza kurasa nyingi za gazeti hili.

Kwa kutazama hilo, tunaweza kusema kuwa hiyo ni ama sadfa, bahati au kujirudia kwa historia. Ni rahisi kuamua haraka kiasi hicho. Haijulikani kama ni historia ilijirudia ama vinginevyo, lakini angalau tunaweza kukubaliana kuwa hiyo ndiyo hali halisi na ya wazi.

Post a Comment

0 Comments