The Crow :Kazi ya mwisho ya Brandon Lee

KUNA filamu ambayo ilitolewa baada ya mhusika kufa, The Crow.
Ingawa katika umaliziaji wa filamu ufundi mkubwa ulifanyika, picha hii ni moja ya picha zilizoonesha utamu wa uigizaji wa Brandon Lee.
Filamu hii iliyotoka mwaka 1994  na kuongozwa na  Alex Proyas ni filamu ya kufikirika, yenye aksheni babu kubwa na yenye ladha ambayo mchanganyiko wake ni tishio la ubunifu wa mambo ya kufikirika  na ukweli.
Ikiwa imeandikwa na  David J. Schow na John Shirley kutoka katika kitabu cha The Crow cha komiki kilichoandikwa na  James O’Barr inazungumza habari za Eric Draven mwanamuziki wa mitindo ya roki ambaye anafufuliwa ili kulipa kisasi cha kifo chake na cha mpenzi wake.
Nafasi ya Draven iliyochezwa na Brandon Lee, kiukweli aliuawa kwa bahati mbaya wakati wa utengenezaji wa filamu .
Ingawa hii filamu ilichelewa kutoka kutokana na kifo cha Brandon,The Crow ilipokewa vyema na wapenzi wa sinema kutokana na mfumo wa usimuliaji wa hadithi na picha zenyewe.
Simulizi linasema Oktoba 30 katika mji wa Detroit, Michigan watu walichoma moto majengo, huku sajini Albrecht (Ernie Hudson) akiwa katika eneo hilo ambapo Shelly Webster (Sofia Shinas)  amepigwa na kubakwa huku mchumba wake, mpiga gita Eric Draven (Lee), akiwa ameuawa.
Wawili hao walitaka kuoana siku inayofuata.Wakati akiondoka kuelekea hospitalini na Shelly, Albrecht anakutana na  binti mdogo ambaye alikuwa anatunzwa na akina Eric, Sarah (Rochelle Davis). Albrecht  anamwambia kwamba kila kitu kitakuwa sawa, akijua si sawasawa.
Mwaka mmoja baadae, Sarah anazuri makaburi ya Eric na Shelly. Huku akiondoka kunguru anatua katika jiwe lenye ishara ya kaburi la Eric na kufanya kitendo kama cha kugonga.
Eric anaamka kutoka katika kifo chake na kutoka kaburini akiwa anatetemeka. Eric anamfuata kunguru huyo hadi nyumbani kwake na kuona hakuna mtu.
Pale anakutana na paka wake Gabriel. Eric  anarudi  siku ya mauaji yake na mchumba wake na kubaini kwamba aliyefanya mauaji hayo ni  T-Bird (David Patrick Kelly), Tin-Tin, Funboy, na Skank (Angel David), ambao wanamfanyia kazi Top Dollar (Michael Wincott) na mapenzi wake ambaye ni dada yake wa kambo Myca (Bai Ling).
Eric  katika vurugu kubwa za kulipiza kisasi alipata msaada mkubwa kwa kunguru yule ambaye naye dakika za mwisho nusura afe, lakini akapona na kumrejesha Eric katika uwezo wake.
Sinema hii ilimpatia umaarufu sana Brandon lakini hajawahi kuwapo kuona utamu aliouigiza hasa kutokana na simulizi la kunguru Yule ambaye walikuwa wanaunganishana kitelepathi  kiasi cha kumfanya aendelee kuadhibu wale wahuni hadi mwisho.
Mkali huyu alizaliwa Februari 1, 1965 Oakland, California,  Marekani na alitumia miaka minane ya maisha yake akiwa na wazazi wake mjini Hong Kong.
Ni mtoto wa Bruce Lee na Linda Lee Cadwell. Ni kaka yake Shannon Lee.  Alijifunza mapigano ya kujihami ya kung fu kama baba yake.  Akiwa katika chuo cha Boston, Massachusetts Mwaka 1983 alitimuliwa shule kwa sababu ya tabia mbaya lakini baadaye akapata diploma yake Miraleste .
Aliigiza Rapid Fire (1992), Showdown in Little Tokyo (1991) na hii ya The Crow (1994).  Mkali huyu ambaye alikufa akiwa na miaka 28 wakati wa utengenezaji wa sinema ya Crow (1994) alikufa Machi  siku kadhaa kabla ya kuoana na Eliza Hutton  Aprili 17, 1993.  amezikwa karibu na baba yake katika makaburi ya Lake View Cemetery.

Post a Comment

0 Comments