Kama kazi yako imekushinda usiendelee kuniuliza maswali ya kitoto. Carlos alikemea kwa sauti kali huku akikuna ndevu zake ambazo tayari zilianza kuota mvi.
Jaji wa mahakama kuu ya Ufaransa, Prof. Olivier Laurent akamwamuru kwa mara nyingine tena ajitambulishe kwa usahihi jina na kazi yake.
Mbweha (The jackal) kwanza akatabasamu kwa dharau ya wazi, akageuka kushoto kumtazama mwanasheria wake mama Isabelle Peyre (ambae baadae kidogo alikuja kumuoa na kuwa mkewe wa tatu), kisha akafungua kinywa chake akasema "Mimi ni muongeaji mzuri sana, ni jambo la kipuuzi ikiwa wewe jaji pamoja na mahakama yako tukufu mmeshindwa kuligundua hilo. Haina haja ya kuendelea kaniuliza mimi ni nani, zunguka ulimwengu mzima, uliza mimi ni nani, wananifahamu vizuri. Kuhusu swala la kazi yangu, hakuna mpumbavu japo mmoja asiyetambua kuwa mimi ni mtaalamu wa mapinduzi (professional revolutionist)".
Carlos akiwa amezungukwa na askari siku ya hukumu yake.
Kwa mara nyingine tena ya tatu, Carlos alipatikana na hatia na kuhukumiwa kuozea jela.
Baada ya hukumu hii aliongea na mwandishi wa BBC kwa kufedheheka sana akasema "Ni muujiza nipo hai hata leo, Mungu ni mzuri sana, nimesalimika kuingia kuzimu katika mapambano mengi sana dhidi yangu, hata hili nalo halitanishinda. Naumia sana sijawahi kuwa baba mzuri kwa binti yangu Elba Rosa, wala mume mzuri kwa mke wangu. Kitu kinachoniuma zaidi rafiki yangu Raisi wa Venezuela Hugo Chavez hanitumii tena sigara tamu, siruhusiwi tena kuzungumza na wafungwa wenzangu. Naamini nikitoka jela nitakutana tena na Fidel Castro tugonge mvinyo wa ikulu"
Hugo Chavez aliwahi kusema "Carlo is a distinguished compatriot"_ "Carlo ni jembe langu la uhakika"
Carlos the jackal ni nani?
Tarehe 12 Oct 1949 mwanasheria nguli wa Venezuela Jośe Ramiréz na mkewe Elba Maria walifanikiwa kupata mtoto wa kiume katika kitongoji maarufu cha Tachira. Bwana Jośe Ramurez alikuwa ni mtu aliyeshikilia mno msimamo na itikadi kali za Umaski (Marxism) hivyo aliwaita wanae wote watatu kwa ukumbusho wa kiongozi maarufu wa Urusi raisi Ilyich Lenin Vladimir aliyeshikilia haswa itikadi ya Umaski. Mwanae wa kwanza ambaye ndio Carlos alimuita Ilyich Sanchez Ramirez, mwanae wa pili Lenin na watatu Vladimir.
Kutokana na uwezo wa kifedha wa baba yake, Sanchez (Carlos) alibahatika kwenda shule mbali mbali zenye hadhi nzuri kielimu. Carlos hakupenda kabisa masomo ya kawaida, alipofika tu miaka 15 Sanchez aliamua kujiunga na vuguvugu la vijana wa chama cha kikomunisti cha Venezuela. Ambapo mara kadhaa walifanya fujo, maandamano na ghasia kupinga uongozi wa chama tawala.
Akiwa na miaka 17 baba'ke aliamua kuongozana nae kushiriki katika mkutano mkuu wa Umoja wa mabara matatu (tricontinental conference), mkutano uliohusisha mabara ya Africa, Asia na Amerika Kusini.
Kwa mara ya kwanza Sanchez alipata uhalisia wa jinsi dunia inaendeshwa ambapo aligundua kua nchi za bara la Ulaya na Marekani zilitumia resources zilizokua nazo kunyonya nchi za dunia ya tatu (3rd world countries).
Hapa ndipo sumu ya mapinduzi ilipoanzia. Mara baada ya mkutano wa umoja wa mabara matatu kuisha, Sanchez alimuomba baba yake ampeleke shule ya mafunzo ya kijeshi.
Jan 1966 akiwa amebakiza miezi kadhaa afikishe miaka 18 baba'ke aliamua kumpeleka chuo cha mafunzo ya vita vya porini (guerilla warfare) kinachoendeshwa na shirika la kijasusi la Cuba (Cuban DGI) nje kidogo ya mji mkuu wa Cuba, Havana.
Mwishoni mwa mwaka huo wazazi wake walitengana. Mama yake akaelekea London na watoto wote, ambako alikua akiendelea na masomo katika chuo cha Staffort. Mwaka 1968, Sanchez akiwa na miaka 19 alichukuliwa na babake akasome Paris, Ufaransa, lakini Sanchez aligoma kabisa na kupendekeza apelekwe chuo kikuu cha Patrice Lumumba kilichopo Moscow mji mkuu wa Urusi. Kwa mujibu wa BBC, chuo hiki kiliasisiwa kwa malengo ya kuandaa viongozi wenye misimamo mikali ya kikomunisti hasa wa nchi za dunia ya tatu. Chuo hiki kimepika viongozi wa juu wa nchi mbali mbali za Afrika ikiwemo Sudan, Namibia, Benin, Afrika ya kati nk.
Kutokana na tabia za ukorofi, fujo, utukutu, uhuni na kuishi kiPlayboy alichukiwa sana na wakufunzi. Mwaka 1969 Sanchez aliandaa maandamano ya wanafunzi wa kiarabu nchini hapo, kosa lililomfukuzisha chuoni hapo.
Picha ya passport ya Carlos iliyopo kwenye vyeti na hati yake ya kusafiri.
Mwaka 1970 Sanchez alitimkia Palestine, ambapo alijiunga na kikundi maarufu sana miaka ya 70 kilichoitwa Chama Mashuhuri cha Ukombozi wa Palestine (Popular Front for Liberation of Palestine-PFLP). PFLP kilikua ni kikundi cha kigaidi kilichojificha chini ya mwamvuli wa multipartism, ambacho kilikuwa kikidhaminiwa na KGB (Taasisi ya Urusi ya Ulinzi na Ujasusi), kikundi hiki kilianzishwa mahsusi kwajili ya kuleta vurugu nchini Israel ili kudhoofisha usalama wa taifa hilo.
Akiwa PFLP Sanchez alipata mafunzo ya daraja la juu ya ugaidi, vita vya porini, silaha na mbinu za kijeshi. Sanchez alionesha uhodari mkubwa sana hasa katika shabaha, ukakamavu na kupika mipango ya uvamizi na utekaji.
Sept mwaka huo Kikundi cha shirika la ukombozi wa Palestine (Palestine Liberation Organisation) chini ya Yasser Arafat kiliingia mgogoro na jeshi la nchi ya Jordan, hivyo kuibuka vita maarufu iliyopewa jina la September nyeusi (Black September). Chama cha PLO kilipozidiwa nguvu baada ya mapambano kikaomba msaada wa kijeshi kutoka kwa kikundi cha kina Sanchez, PFLP.
Akiwa kijana mdogo kabisa wa miaka 21 aliteuliwa kuongoza kikundi cha PFLP kipambana vita ya Black September. Bwana mdogo alibadili kabisa upepo wa vita hiyo, jeshi la Jordan liligaragazwa vibaya mno, Sanchez alichora mbinu za uvamizi zilizowachanganya maadui. Alibuni magwanda ambayo yalifanana sana na yale ya jeshi la Jordan, akachora ramani ya kutengenga mitaro ya chini kwa chini (tunnels) kutoka walipoweka kambi hadi walipo jeshi la Jordan, walifika eneo la tukio usiku na kisha kujichanganya na wanajeshi wa Jordan. Baada ya hapo mashambulizi yanaanza.
Mbinu hii ilifanikiwa sana mpaka Mfalme wa Jordan Hussein akaomba maridhiano. Bado Sanchez hakuridhika, akasuka ramani za kuteka ndege zilizotua Jordan. Mwezi huo huo September alifanikisha utekaji wa ndege nne zilizotua Jorsani zikiwemo SwissAir, TWA , Azraq na BOAC.
Uhodari katika vita hii ya black September ndio ulimfanya Sanchez abatizwe jina la Carlos, ambalo ni maarufu nchi za Amerika Kusini kumaanisha 'Mwanaume shujaa'
Kiongozi mkuu wa PFLP Generali Wadie Haddad alifurahishwa na umakini wa Carlos hivyo kuamua kumpeleka London akapate mafunzo ya juu zaidi ya kijeshi. Mwaka uliofuata 1971 Carlos alienda mafunzoni London na ndipo alianza matukio ya kigaidi.
Bingwa wa mission impossible katika karne ya 20.
Akiwa Uingereza 1971, alipanga nyumba ya kawaida nje kidogo ya jiji la London, alitumia miezi minne kubuni na kufunga systems za usalama kwajili ya ulinzi wa nyumba yake. Kutendo hiko kilipelekea askari kumtilia mashaka. Polisi kadhaa walifika nyumbani kwake kufanya upelelezi ili kufahamu nini hasa Carlos anakusudia. (Ikumbukwe kua jina la Carlos lilikua maarufu sana lakini hakuna aliyemtambua kwa sura). Baada ya upelelezi, polisi hawakufanikiwa kumkuta na kosa lolote.
● 26 Oct 1972, Carlos alifoji passport ya Costa Rica na kutoka Uingereza kuelekea Damascus mji mkuu wa Syria. Alifanya hivyo kuwachanganya polisi, yani documents zioneshe bado yupo Uingereza wakati yupo Syria. Tarehe 27 na 28 akasuka ramani ya utekaji, akawaandaa wenzake wawili. Tarehe 29 wakaingia uwanja wa ndege wa Damascus, saa 6 mchana ndege ya Lufthansa (Boeing 727-100) iliyokua inaelekea Frankfurt, Ujerumani ikatekwa nyara.
Carlos akatuma salamu kwa raisi wa ujerumani kupitia Waziri wa ulinzi Dr. Theodore Blank. Serikali ikamwomba sana Carlos awaache mateka wakiwa salama kwa gharama yoyote ile. Carlos akamwamuru kua kila mateka matatu ni sawa na mfungwa mmoja wa PFLP aliyefungwa Ujerumani hivyo anataka wafungwa waachwe huru. Makubaliano yakafikiwa kwa pande zote mbili.
Carlos akamwamuru rubani apaishe ndege kuelekea Zagreb, Croatia. Mateka wote wakashushwa wakiwa salama kisha ndege ikarushwa hadi Tripoli, Libya. Carlos na wenzake wakapewa hifadhi na Gadaffi. Keshowe tarehe 30 Carlos akarudi zake London.
● Siku 3 baadae mashindano ya Olympics yalianza nchini Ujerumani. Kundi la Black September lilimuomba Carlos awasaidie kutekeleza shambulio litakalopeleka ujumbe kwa dunia kuhusu unyonywaji wa taifa la Palestine. Carlos aliunda shambulio hatari ambalo leo hii ni maarufu kwa jina la mauaji ya Munich (Munich Massacre). Lakini Carlos hakutaka kushiriki kwenye shambulio hilo, alikaa pembeni.
Tarehe 5 Sept wanaOlympic 11 wa Israel walitekwa na kuuwawa na Black September. Wote waliohusika na mauaji hayo waliteketezwa mmoja baada ya mwingine kwa nyakati tofauti na shirika la ujasusi la Israel, MOSSAD. Lakini Carlos alibaki anadunda tu London.
Taarifa za siri zilizovijishwa na WikiLeaks zinadai kwamba MOSSAD hawakuweza kumuuwa Carlos kwamba hakuwa na hajawahi kuwa tishio kwao.
● Bado akiwa mafunzoni London, Nov mwaka huo huo Carlos alipiga tukio la kushtukiza ambapo katika siku 1 kulikua na uvamizi wa mabomu katika benki ya Israel tawi la London na kituo cha gazeti 1 maarufu la Israel. Magari na majengo yaliharibika lakini hakukuripotiwa vifo wala majeruhi. Baada ya shambulio hiyo ndipo Carlos aliingia rasmi kwenye ligi la wababe Ulaya, akateka rasmi attention ya vyombo vya ulinzi na usalama.
● Dec 30 1973, Carlos aliamka mapema kabisa, akafungua briefcase, akashika mafuta na kitambaa akasafisha pisto yake aina ya Tokaruv, kisha akahesabu risasi 4 akazitia kwenye magazine. Akachukua sigara akavuta vipisi viwili kisha safari ya kuelekea nyumbani kwa Josef Sieff ikaanza.
Josef Sieff alikua mfanyabiashara mkubwa Uingereza mwenye damu ya kiyahudi na pia alikuwa mwenyekiti wa shirikisho la kizayuni la Uingereza (British Zionist Federation), huyu jamaa mara kadhaa alitoa matamko ya kulaani viongozi, vyama vya ukombozi na wananchi wa Palestine.
Alipofika alikua na kibali cha kufoji kilichomwezesha kuruhisiwa na walinzi kuingia. Baada ya kuingia ndani alikutana na binti wa kazi wa Josef, akamuomba aoneshwe alipo Josef. Alimkuta Josef akiwa bafuni anaoga, alichokifanya ni kuchuchumaa na kuchomoa pisto yake aliyoificha kwenye soksi, akachukua target na kuachia risasi moja ambayo alienda moja kwa moja usoni mwa Josef, bahati mbaya/nzuri ilimpunyua kati ya pua mdomo (upper lip). Carlos akajaribu kuvuta risasi ya pili bahati nzuri/mbaya akashtuka risasi zimejam kwenye silaha. Bila kupoteza muda akatoroka haraka sana na kumwacha Josef mahututi.
Nyumba ya Josef
Keshowe taarifa zilisambaa zikimuonesha kiongozi wa muda wa PFLP akisisitiza kuwa shambulio hilo ni kulipa kisasi kwa Israeli baada ya MOSSAD kumuuwa kiongozi mmoja wa juu wa PFLP Mohammed Boudia.
Baada ya tukio hilo Carlos akakimbia London na kuelekea Palestine.
● Shambulio lililofuata halikuwa rahisi. Mpango ulikuwa ni kulipua kwa kombora (rocket-propelled grenade) ndege 2 za israel za El Al zilizokua zikitua uwanja wa Orly karibu na Paris. Mashambulio haya yalifanyika kati ya tarehe 13 na 15.
Mashambulio haya hayakufanikiwa kama ilivyopangwa, yalisababisha uharibifu wa ndege bila kifo wala majeruhi. Mbaya zaidi, gaidi mwenza wa Carlos Michel Moukharbal alikamatwa na askari wa Ufaransa katika tukio hilo.
Akiwa katika uangalizi mkali alihojiwa kwa kuteswa (enhanced interrogation), hadi alipofunguka na kutoa utambulisho wa Sura, muonekano na tabia ya Carlos ili kufanikisha kukamatwa kwake. Mourkharbal alikubali kushirikiana na kitengo cha ujasusi- DST cha kupambana na magaidi (counterterrorism) ili kufanikisha kukamatwa kwa Carlos.
Moukharbal na maafisa wawili wa Ufaransa walifika nyumbani kwa Carlos. Carlos akiwa chumbani kwake aliwaona vizuri sana kupitia camera za ulinzi, akawapa kibali walinzi wawaruhusu kuingia. Carlos akakutana nao, wakasalimiana vizuri na kuwakaribisha kukaa. Carlos akanyanyuka akawapa juisi na stori zikaendelea.
Walivyomaliza kunywa Carlos akanyanyuka akamwambia Moukharbal, ni salama ukafia mikononi mwangu kuliko kuuwawa na nguruwe wa ulaya, akachomoa bastola akaanza kumuuwa Moukharbal kisha akawamalizia wale majasusi wa Ufaransa kisha akatoroka haraka kuelekea Beirut kupitia Brussels.
Tukio hili lilizagaa dunia nzima, ndipo vyombo vya habari vikambatiza jina la Mbweha (Tha jackal) na kumfanya awe tofauti na Carlos wengine wote duniani.
OPEC siege: Shambulizi la utekaji maarufu zaidi duniani.
Akiwa Beirut ndipo Carlos alishinda usiku na mchana kusuka mission ambayo aliamini vizazi na vizazi havitamsahau, mpango mzima ulikuwa ni kuyaliza mataifa makubwa yanayochimba na kusafirisha mafuta ambapo ndani yake kuna unyonyaji mkubwa kwa mataita madogo.
Ilikuwa hivi...
Jumapili ya tarehe kama ya jana Dec 21 1975 mjini Vienna kulikuwa na mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya nchi zinazozalisha na kusambaza mafuta (Organisation for Petroleum Exporting Countries-OPEC). Mkutano huu ulihudhuriwa na Viongozi wakubwa wa mataifa mbali mbali.
Mkutano wa OPEC 1975
Carlos akiwakilisha kikundi cha PFLP aliongoza timu ya watu 6 hatari katika uvamizi ulioushangaza ulimwengu akiwemo mwanamama nguli Gabrielle Kröcher (huyu alikuwa mwanamke wa kijerumani aliyeheshimika kwa kulenga shabaha kutumia mkono wake wa kushoto) .
Mwanamama Gabrielle Krocher
Asubuhi saa 3 walifika makao makuu ya OPEC ambapo mkutano ulikua unaendelea. Askari wa 4 wa Australia walichangamkiwa mapema sana baada ya kina Carlos kuingia getini, mmoja wa askari hao alifariki papo hapo. Baada ya kuingia ndani, kabla mwajiri mmoja wa OPEC hajabonyeza simu kuwapigia askari, mwanamama Gabrielle alimtuliza kwa shaba 1 ya bega, hapo pia alijitokeza askari mlinzi wa Waziri wa mafuta wa Libya, naye aliwahiwa kabla hajaketa madhara, hivyo kufanya idadi ya vifo kufika watu wa 3.
Kina Carlos wakapata access ya kuingia kwenye chumba cha mkutano kilichokuwa na wajumbe 63 wakiwemo mawaziri 11 wa mafuta wa nchi mbali mbali.
Carlos alichomoa simu ya waziri mmoja wa Austaria, akampigia raisi kumpa taarifa. Carlos alitoa masharti maraisi sana kwa serikali;-
》》Alitaka liletwe basi litakalowabeba mateka wote kuelekea Airport.
》》Alitaka ndege iwepo pindi wakatakapofika airport na iwe full tanked.
》》Alitaka malalamiko yote ya Palestina dhidi ya mataifa mengine yarushwe kwenye televisheni na redio ya taifa ya Australia kila baada ya masaa ma 2.
La sivyo Carlos aliahidi kuuwa mateka mmoja baada ya mwingine kila baada ya dakika 15.
Australia walifahamu vizuri jinsi Carlos alivyo mtata na mwenye uwezo wa kukamilisha matukio kwa weledi mkubwa bila kuacha ushahidi wowote. Hivyo waliamua moja kwa moja kukubali matakwa yote ya Carlos pasipo pingamizi.
Basi lililetwa mara moja, mateka wote na kina Carlos walielekea airport.
Mateka wakielekea uwanja wa ndege.
Keshowe siku kama ya leo tarehe 22, walipewa ndege ya serikali aina ya Boeing, pia Carlos aliamrisha apewe rubani Neville Atkinson. Huyu alikuwa rubani mstaafu wa jeshi la anga la uingereza (royal navy pilot), wakati huo rubani huyo alikua rubani wa Kanali Muamar Gaddafi.
Ndege iliyotumika kusafirisha mateka wa uvamizi wa OPEC
Carlos alimwamuru rubani apaishe ndege kuelekea Algiers, Algeria ambapo aliwaacha huru mateka 20 kwa makubaliano ya kupewa silaha, risasi, pamoja na kujazwa mafuta kwenye ndege. Baada ya hapo alimwamuru rubani apae kuelekea Tripoli.
Baada ya kufika Tripoli Carlos aliwaachia huru mateka 10 kwa makubaliano ya kubadilishiwa ndege apewe ya kifahari zaidi na yenye uwezo mkubwa na pia kuhakikishiwa ulinzi siku nzima kabla hajaondoka.
Tarehe 23 Dec kina Carlos na mateka waliwasiri tena Algiers ambapo aliahidi kuwaachia hai mateka wote iwapo atapewa kiasi cha pesa kisichopungua $50 mil na ahakikishiwe kupalewa hifadhi/maficho (asylum). Ilikuja kugundulika kuwa pesa hii ilitolewa na serikali ya Saudi Arabia na Iran na kwamba Carlos alitumia pesa yote akiwapa wenzake kiasi kidogo sana. Mateka waliachiwa huru baada ya Carlos kujiridhisha kua atapewa ulinzi wa kutosha hapo Algeria.
Hakuna kitu kilichomkera kiongozi mkuu wa PFLP kama shambulio la OPEC. Kwake yeye utekaji huo haukuwa na faidi yoyote kwani lengo walilopanga halikutimia. Kazi kina Carlos waliagizwa kuifanya ilikuwa ni kuwauwa mawaziri wa mafuta wa Saudi Arabia, Ahmadi na Jamshid wa iran. Pia Waddi Haddad alikerwa na kitendo cha Carlos kuchukua pesa zote kwa matumizi binafsi. Hivyo, Haddad ambae pia alikuwa mkufunzi wa Carlos wa maswala ya kijajusi aliamua kumtimua Carlos kutoka PFLP.
Hali ya usalama haikuwa nzuri kwa Carloa baada ya kutimuliwa PFLP, akatorokea Yemen Kusini, kisha akaelekea Libya alipopokelewa na kupewa hifadhi na Gaddafi, ambaye inaaminika ndiye alifadhili shambulio la OPEC (The Libyan Revolution: Its Origins and Legacy : a Memoir and Assessment). Akiwa Libya alijitolea kutoa mafunzo ya mbinu za vita vya porini (guerrilla warfare) kwa wanajeshi wa Jibya.
July 4 1976 ndege ya Ufaransa ilitekwa ikitokea Tel Aviv na kupelekwa Entebbe Uganda, taarifa zilisambaa kila sehemu kua mtekaji ni Carlos japo Carlos mwenyewe alipinga kuhusika na shambulio hilo.
Mwaka 1976 raisi mkorofi wa Iran Mohammad Reza Shah Pahlavi ambaye baadae alipinduliwa na Ayatollah alipata taarifa za kiintelijensia kuwa target kuu ya Shambulio la OPEC lilikuwa ni kumuuwa Waziri wake, hivyo alikasirishwa na kupania kumuuwa Carlos. Alitumia kiasi kikubwa sana cha pesa kuwakodi wauaji hatari wanne wamuondoe Carlos kwenye uso wa dunia. Magaidi hao walikuwa ni:-
>>Manuel Contreras: Huyu alikuwa afisa wa jeshi la Chile na mkurugenzi wa taasisi ya Intelijensia ya Chile (DINA). Huyu jamaa alifariki mwaka jana, akiwa anatumikia vifungo tofauti 59 visivyo na dhamana ambavyo vina hukumu ya miaka 529 kwa ujumla.
>>Garhard Mertins: huyu ni Mjerumani mtaalamu wa kuruka angani kutokea kwenye ndege za kivita (paratrooper). Huyu jamaa ndiye alikua kiongozi wa operesheni Gran Sasso, shambulio lililomtorosha Benito Musolini kutoma gereza mwaka 1943.
>>Sergio Arredondo: huyu jamaa katika naisha yake aliuwa watu 75 kwa mkono wake. Alikuwa kamanda msaidizi wa kikosi cha 'msafara wa kifo' (caravan of death).
Muuwaji wa nne hakuwahi kufahamika lakini inasemekana alikuwa ni Mpalestina.
Hawa wauaji wote kwa pamoja walipanga mashambulizi manne ya kumuuwa Carlos kutekeleza amri ya Shah Reza. Katika mission zao hawakuwahi hata siku moja kumuona Carlos japo taarifa za Carlos zote walikuwa nazo. Mwishowe waliamua kunyoosha mikono juu, wakarudisha mrejesho kwa Shah Reza kua kumuuwa Carlos ni sawa na kupaka rangi upepo.
Viongozi wa juu wa Stasi-Kitengo cha siri cha polisi cha Ujerumani Mashariki, walizikubali harakati za Carlos kwa muda mrefu, baada ya kupata taarifa kuwa hayupo salama, Nov 1976 walijitolea kumpa Carlos hifadhi ya nyumba za kifahari, ofisi kwajili ya kuanzisha kikundi chake kipya, magari pamoja na makomando wa kumpa ulinzi. Jambo la kushangaza zaidi ni kua Carlos aliruhusiwa kutembea na bastola hadi mtaani.
Mwaka 1977 Carlos alianza kuunda kundi lake la kigaidi liitwalo Arab Armed Struggle. March 1978 kiongozi wa PFLP aliuwawa kwa sumu aliyepuliziwa na MOSSAD, Carlos aliwashawishi wanamgambo wa PFLP wajiunge na kundi lake, jambo ambalo halikuwa na utata.
Mwaka 1979 Carlos alifunga ndoa na binti mkali kabisa wa Ujerumani Magdalene Kopp, ambaye pia alikuwa gaidi wa level ya juu sana.
Carlos arejea tena kwenye ligi la wakubwa.
Bado Carlos hakuridhika kabisa na vyote alivyofanya, alihisi hajamaliza kazi iliyomleta duniani. Mwaka 1981 kupitia kikundi chake alirudisha mashambulizi kwa maadui zake wa Ulaya.
Kwanza alianza kuteka makao makuu ya Radio Free Europe yaliyopo Munich. Hakusababisha vifo lakini aliuamsha ulimwengu na kutoa ujumbe kuwa amerudi ulingoni.
Carlos alipata taarifa kua adui yake mkubwa Ufaransa anasuka vinu vya nyuklia. January 1982 alipanga shambulio la kulipua vinu vyote vya nyuklia vya Ufaransa. Katika uvamizi huo mipango haikwenda kama ilivyokusudiwa kutokana na ulinzi mzito uliokua maeneo hayo, hivyo kusababisha mke wa Carlos Magdalene kukamatwa akiwa na gari limejaa mabomu.
Carlos alituma barua ya kutaka Ufaransa wamwache huru mkewe, lakini Ufaransa hawakuwa tayari kutekeleza maombi hayo, wakaendelea kumshikilia. Walijifanya Wamesahau mtu gani wanaeshindana nae.
Carlos akiwa kwake Beirut alipata hasira kudharauliwa na Ufaransa. Akaanzia hapo hapo Beirut, tarehe 15 March mwaka huo akavamia kituo cha utamaduni cha Ufaransa kilichopo Beirut, akalipua jengo zima ambalo mpaka kesho Wafaransa wameshindwa kulinyanyua.
Week 2 baadae Carlos akapaa kuelekea Paris, Ufaransa akitumia passport ya Uingereza. Siku hiyo raisi mstaafu wa Ufaransa Jacques alikua akisafiri kutoka Paris kuelekea Touluese, na Carlos alipata taarifa kuwa raisi atatumia usafiri wa treni. Target ya kwanza ya Carlos akiwa Paris ni kuteka treni hilo, kisha akalipua kwa bomu, shambulio lililosababisha vifo vya maafisa watano wa serikali na majeruhi zaidi ya 77. Bahati nzuri raisi mstaafu alihairisha safari yake.
Siku hiyo hiyo Carlos na timu yake walilipua gari la gazeti la Al-Watan Al-Arabi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 63.
Dec 31 1983 Carlos aliukaribisha mwaka 1984 kwa furaha kubwa, alitekeleza shambulio jingine hatari Ufaransa. Aliteka na kulipua stesheni ya treni na magari ya Marseille Saint-Charles, watu wawili walifariki na 33 kujeruhiwa.
Siku hiyo hiyo treni itokayo Marseille kuelekea Paris nayo ilitekwa na kulipuliwa, shambulio lililosababisha vifo vya watu watatu na 12 kujeruhiwa.
Siku hii isingeisha bila kulipua Maison de France iliyopo Berlin, Ujerumani na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 22.
Keshowe siku ya sherehe ya mwaka mpya, Carlos alituma ujumbe kwa vituo vitatu vya habari watangaze kua mashambulio yote hayo matatu yeye ndiye anahusika kama ishara ya kulipa kisasi.
Wafaransa bado walishikilia msimamo wake wa kutomwachilia mkewe, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela. Carlos nae hakuvumilia, akashusha tena shambulio jingine ambapo alilipua duka la bidhaa (shopping mall) Paris.
Carlos aliendelea kuwatesa Ufaransa hadi ilifika kipindi pesa maalumu ikatengwa kwenye bajeti ya Ufaransa kwajili ya kuongeza vifaa na ufanisi ili kumkamata Carlos, vyote hivi havikusaidia.
Mpaka kufika hatua hii, Carlos alikua adui namba moja wa dunia (most wanted fugitive).
May 4 1985, mke wa Carlos Magdalene Kopp aliachwa huru baada ya kuonesha nidhamu ya kuridhisha, kisha akaungana na Carlos nchini Hungary.
Kipindi hiki hakikuwa kizuri kwa Carlos, kwani alikuwa amefulia vibaya sana kutokana na kufariki kwa raisi wa Iraq ambaye alikua ni jamaa yake wa karibu, pia hali ya uchumi wa Libya ulikua umedorora sana hivyo Gaddafi hakuweza kumfadhili tena.
Hali ya usalama wake haukuwa mzuri, hivyo aliamua kukimbilia Syria, Aug 17 1986, mkewe akajifungua mwanae wa kwanza. Wakiwa Syria, waziri wa Ulinzi ulimuomba sana Carlos atulie, aache matukio ya ugaidi na ikiwezekana astaafu kabisa, lasivyo Syria isingekuwa tayari kuendelea kumlinda.
Hiki kilikuwa Kipindi kigumu zaidi kwa Carlos, miaka mitano bila kufanya shambulio. Kama wasemavyo waswahili "Jasiri haachi asili".
1990 serikali ya Iraq chini ya Saddam Hussein alimfata Carlos Syria wafanye kazi. Mpango mzima ulikuwa ni Iraq kuishambulia Kuwait. Carlos asingeweza kukataa dili hilo, akalamba dola mil 2 ya Saddam kama advance ya makubaliano ya dola mil 5.
Mipango ya Saddam hussein ilivuja kwenye mashirika ya usalama na ujasusi ya Ulaya ikiwemo DGSE ya Ufaransa. Hali hii ilitishia usalama wa Carlos hadi kumlazimu akimbilie Sudan ambapo aliishi kwenye handaki huko Khartoum.
Kukamatwa kwa Carlos.
Akiwa Sudan taasisi za kijasusi za Ufaransa, DGSE na Marekani, CIA zilitangaza dau kubwa sana kwa utawala wa Sudan kama wangefanikisha kukamatwa kwa Carlos. Sudan hawakuwa na ujanja wa kukataa.
1994 Carlos alifanyiwa upasuaji mdogo kwajili ya ugonjwa wa tezi dume katika hospitali ya taifaya Sudan. Siku mbili baada ya upasuaji, maafisa wa usalama wa Sudan wakamtaarifu Carlos kwamba anabidi ahamishwe kwenda makazi mapya wakihofia shambulio la kifo lililopangwa kumuuwa, pia waliahidi kumpa ulinzi binafsi.
Carlos hakukataa. Usiku huo mlinzi mmoja ambaye alikuwa afisa wa usalama alimvizia na kumchoma sindano ya usingizi na kukata mawasiliano ya mwili kwa masaa 24.
Usiku huo serikali ya Sudan ikawasiliana Waziri wa ulinzi wa Ufaransa kwamba Carlos yupo chini ya mikono yao. Alisafirishwa usiku huo huo kuelekea Ufaransa. Keshowe Carlos alipata ufahamu akiwa amezengukwa na maafisa wa usalama wa Ufaransa Paris, mikono na miguu yote imezungushwa pingu.
Hukumu
Dec 1997 Carlos alipatikana na hatia na kushtakiwa kifungo cha maisha bila parole.
Mwaka 2001 Carlos aliamua kumrudia Mungu, na kuwa Muislam. Mwaka huo huo akamuoa mwanasheria wake Isabelle ambae ni wakili nguli sana.
Akiongea kutoka chumba chake cha magereza, Carlos alimtaja Bin Laden kuwa mrithi wake katika vita dhidi ya ubeberu (imperialism) wa mataifa ya magharibi.
Kanali Muamar Gaddafi aliwahi kusikika akisema "Marekani ni nchi yenye nguvu sana, si kama Libya ama Iraq, lakini ukiamua kuwaonesha kuwa unachukizwa na matendo yao, mtoe Carlos jela, mwekee bastola mezani mpe pesa na sigari...kisha washa TV ufuatilie breaking news"
Huyu ndiye mbweha Carlos, Ilyich Sanchez Ramirez mtaalamu wa mapinduzi aliyeitikisa dunia kwa miongo mitatu.
0 Comments