Ziara Ya Che Guevara Zanzibar

Picha hii muhimu ilipigwa baina Feb na April 1965 wakati Che alipowasili Dar kwa maandalizi ya kwenda Congo kuwaunga mkono vikundi vya kina Kabila dhidi ya utawala wa dikteta Mobutu.Tarehe 11 Feb Che alizuru Zbar na Mzee Karume akamkabidhi mgeni huyo kwa Ali Sultan huku akimueleza "Sikiliza Ali! Nakukabidhi mgeni huyu 'comrade' mwenzenu uwe nae wakati wa ziara yake hapa Zbar na umhudumie vizuri".Karume hakuwa akielewa uzuri kuwa Che alikuwa tayari anajuana kwa karibu sana na Ali Sultan tangu 1961 kule Cuba wakati ZNP walipokwenda kufungua ofisi Havana.Akaibuka yule shawishi hayati Musa Maisara ikawa kama yeye ndie anaemjuwa na kukabidhiwa mgeni.Kila picha alopiga Che yeye alijiweka ubavuni mwake eti na yeye 'comrade'!

Usiku wa tarehe 12Feb Che alikutana na makomred waliokuwepo Cuba 1962 katika karamu maalum.Siku hiyo walikuwepo Ali Mahfoudh(inasemekana karamu ilifanywa kwake,Migombani),Moh'd Ali Foum,Ali Abdalla Bafakih,Salim Ahmed n.k.

Bahati mbaya makomred wa jeshini wote walikuwa wamepelekwa Urusi (sijuwi kama Jiwe na Ali Mshangama walikuwa tayari wameshapelekwa Indonesia).Kwani Che aliwaulizia na alisikitika sana kuwakosa kuonana nao.Che alipewa nyumba ya kukaa na Ali Sultan pale Beit-Ras nyumba ambayo aliwahi kukaa Mr Amour Ali Amer na hadi leo imewekewa kibao cha kumbukumbu (plaque) ya ukaazi wake kwenye nyumba ile.

  Ziara ya Che Zbar ndio hasa iliyofichuwa habari kuwa Mwanamapinduzi huyo alikuwa Tanzania kwani kabla hapo hakuonekana popote rasmi.Ilifika hadi Balozi wa Marekani Dar kulalamika kwa Nyerere kuwa walikuwa na Intelligence kuwa Babu alikuwa pamoja na Commandante huyo.Mwalimu bila shaka alijua kuwa Che yuko in town lakini alijifanya hajui na eti kumuuliza Babu endapo kweli yuko nae mtu huyo! Janab nae aliruka na kusema kuwa hakumtia machoni mwake.Inasemekana Che aliondoka Dar kwenda msituni Congo mnamo wiki ya mwisho ya mwezi Apri 1965 na alikaa huko hadi Oktoba 1965 yaani miezi kama sita.Aliporudi Dar alijifungia ndani ya jengo la Ubalozi wa Cuba hadi Feb 1966 akiandika Diary na kumbukumbu zake huko Congo.Ni mtu mmoja tu ndie alikuwa akijuwa uwepo wa Che Dar kipindi hicho chote.Nae ni Al-marhum Janab ambae alikuwa ni muekaji siri mzuri katika mambo haya ya struggle.Nakumbuka hata mimi mwenyewe nipokuwa najiandaa ku-infiltrate across mto Ruvuma kwenda msituni Mozambique na vikosi vya Frelimo (1968) mtu pekee ambae alikuwa akijua hatari hiyo alikuwa Babu kwasababu tulikatazwa kueleza kwa yeyote na viongozi wa Frelimo. Hata Serikali ya Tanzania ilikuwa haijuwi.Mimi nilimdokezea just in case endapo nitapotea akamno'goneze baba yangu.Naam alificha siri mpaka tumerudi baada ya miezi 3 porini.Na hapa lazima niseme sisi katika ujana ule tulikuwa 'inspired' na Che Guevara.

Post a Comment

0 Comments