Rais Mstaafu awamu ya Nne Dr Jakaya Mrisho Kikwete, Ambaye pia ni Mkuu wa chuo kikuu cha Dar es salaam, amewataka watafiti kutoka katika chuo hicho kuvumbua zaidi masalia ya wanyama na vitu mbalimbali katika eneo la Tendegulu Mkoani Lindi ili kuvutia watalii lakini pia kuendelea kushikilia rekodi katika nchi zilizoweza kuvumbua mali na viumbe wa kale.
Akizungumza katika ziara yake kwenye eneo la TENDEGULU mkoani Lindi, aneo ambalo mabaki ya mjusi mkubwa anayefahamika kama DINOSARIA yalipatikana mwaka 1908, anasema kama nchi haikuwa imeendelea wakati huo na waliweza kuvumbua mabaki, basi ni wakati wa nchi kuwekeza nguvu kubwa kwenye tafiti ili waweze kugundua mabaki mengine zaidi kwani anaamini mjusi mkubwa aliye nchini ujerumani kwenye makumbusho lazima atakuwa na wenzake ambao bado hawajaonekana nchini.
Aidha, kutokana na kuwepo kwa mali kale adhimu katika eneo hilo, Dr Kikwete ameahidi Rasmi kuwepo kwa ujenzi wa makumbusho ya Taifa ili taarifa na mabaki ya kale yatakayopatikana katika eneo hilo viweze kutunzwa na kuhamasisha utalii kwani eneo hilo ndipo anapotoka mjusi mkubwa duniani ambaye kwa sasa makazi yake ni Nchini Ujerumani.
Wataalamu kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam, wameeleza sababu zilizosababisha wanyama hao wakubwa kutoweka huku wakieleza kubusu jitihada zao ili kuhakikisha masalia mengine yanaendelea kupatikana. Kupitia tafiti kadhaa zilizofanywa Duniani, wataalamu wamehisi chanzo cha wanyama hao wakubwa kupotea duniani ni kimondo kikubwa kilichodondoka miaka mingi katika maeneo ya bahari ya MEXICO YA SASA. Kimondo kilichosababisha mtikisiko mkubwa ulioua zaidi ya asilimia 70 ya wanyama huku jua na maji mengi kujaa baharini suala linalohisiwa pia kuchangia vifo kwa wanyama barani Afrika.
Naye mbunge wa jimbo la Mchinga Bi Salma Rashid Kikwete, ameonya na kuwakumbusha watafiti kuhusu suala la ushirikishwaji ili jimbo litambue ni jambo gani linaendelea katika maeneo yote yanayofanyiwa tafiti. Huku akisema kuwa tafiti na vumbuzi hizo za wanyama wa kale katika jimbo lake la Mchinga, vitakuwa chanzo kikubwa cha mapato yatokanayo na utalii.
Wananchi pamoja na viongozi wa eneo hilo, wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara ambayo kwa sasa inapitika kwa shida. Kutokana na eneo hilo kutabiriwa kupokea watalii wengi, wameiomba serikali iboreshe miundombinu hiyo ili iwe rahisi kwa yeyote atakayependa kutalii na kujifunza aweze kufika kwa Urahisi.
Naye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mheshimiwa Frank Magari, ameomba ujenzi wa eneo la makumbusho uharakishwe ili wananchi wa Lindi na Watalii waweze kujifunza kuhusu mali kale na mabaki ya wanyama watakaopatikana katika eneo la Tendegulu.
Katika eneo la Tendegulu, viongozi na wananchi wamefanikiwa kuona mabaki mengine ya wanyama wa kale ambayo bado hayajakamilika. Huku zoezi la kupanda mlima ambao ni eneo mojawapo ambalo mjusi mkubwa alipatikana, mlima unaobeba historia na kuonyesha ukingo wa zamani wa bahari ambapo kwa karne hii bahari imesogea umbali mrefu kutoka kileleni hapo, kwa sasa imebaki historia ya mabaki ya mawe ya baharini ambayo yanathibitisha kuwepo kwa upwa katika miaka mingi iliyopita.
0 Comments