Maisha baada ya tukio la Copper

"MAISHA BAADA YA TUKIO LA D.B COPPER"
Baada ya tukio la utekaji la Cooper kutokea na FBI
kuonekana dhahiri kuwa wameshindwa kufikia
mwisho wa kutengua kitendawili cha tukio hili hali
ilikuwa tete katika viwanja vya ndege na
kusababisha marekebisho mengi ya protokali za
ulinzi na utoaji huduma katika viwanja vya ndege
nchini marekani.
Kwanza kabisa serikali ya marekani ilitilia mkazo
uanzishwaji upya na kuboresha programu ya
maaskari wanaosindikiza ndege za abiria (Sky
Marshal Program).
Pia serikali ilichukua hatua kali zaidi kwa mara ya
kwanza kabisa kuanzisha mpango wa kupekua mizigo
ya abiria kabla hawajapanda kwenye ndege. Hatua
hii ilisababisha mvutano mkali kati ya wananchi wa
marekani na serikali yao katika miaka ya sabini
ambapo ilifikia hatua kesi za kikatiba zilifunguliwa
dhidi ya serikali ya marekani kwa madai ya kwamba
kupekua mizigo ya abiria ilikuwa inavunja Kipengele/
Marekebisho ya Nne ya katiba ya marekani (Fourth
Amendment) kipengele kinachomlinda raia wa
marekani dhidi ya upekuzi na kuingiliwa faragha
yake. Lakini mwishoni serikali ilishinda kesi hizi na
tangu hapo imekuwa ni jambo la lazima kwa mizigo
kukaguliwa kabla ya abiria kupanda ndege.
Si hivyo tu, serikaki kupitia idara ya usafiri wa
anga nchini marekani (FAA) ikaenda mbali zaidi kwa
kuzitaka kampuni zote za usafiri wa anga
zinazotumia ndege aina ya Boeing 727 wafunge
kifaa maalum cha kuzuia mlango wa nyuma mkiani
mwa ndege kufunguka pindi ndege ikiwa angani.
Kifaa hiki kilipewa jina 'Cooper Vane'.
Na pia FAA walitoa maagizo kuwa ndege zote
ziwekwe matundu maalum ya kuchungulia
(peepholes) katika mlango wa chumba cha marubani
ili kuwawezesha waweze kuona kinachoendelea
upande wa abiria.
Pia, mwaka 2013 Earl Cossey mmliki wa kituo cha
kufundisha Skydiving sehemu ambapo maparashuti
manne yaliazimwa na FBI na kumpa Cooper mwaka
1971 alikutwa ameuawa nyumbani kwake. Bw.
Cossey alikuwa ameajiriwa na FBI mara tu baada ya
tukio la Cooper akiwa kama mshauri muelekezi
(consultant) katika juhudi za kumtafuta Cooper na
alihusika katika hatua zote za upelelezi.
Ziko nadharia nyingi zinazoamini kuwa vyombo vya
usalama vya marekani vinahusika katika kifo cha
Cossey na watu wanadhani kuwa kuna jambo la siri
ambalo alikuja kulibaini katika upelelezi huo wa tukio
la Cooper na FBI walihofia labda Bw. Cossey
asingeliweza kutunza siri hiyo, hivyo basi suluhisho
jepesi wakaona ni kumwondosha.
Hatimae..
Mwezi July mwaka huu 2016 tarehe 14, shirika la
upelelezi la FBI walifunga jalada la kesi ya Cooper
na kukivunja kikosi kazi maalum cha kuchunguza
tukio la Cooper (Cooper Research Team) kwa madai
kuwa haukukuwa na tumaini lolote la kufikia
hitimisho katika upelelezi huo.
Walifunga jalada wakiwa bado hawafahamu kama
Cooper yuko hai au ameshafariki, hawajui kama hilo
ni jina lake halisi au la kubuni, hawafahamu fedha
alizopewa zimekwenda wapi na wala hawafahamu ni
namna gani binadamu mmoja alifanikiwa kutekeleza
tukio kwa usahihi wa asilimia mia moja kama tukio
hili.
Tukio la Utekaji la Cooper ndilo limeingia kwenye
orodha ya kumbukumbu ya shirika la FBI kama Kesi
iliyotumia muda mrefu zaidi kufanyiwa uchunguzi
(miaka 45) na tukio hili limeingia kwenye vitabu vya
historia ya nchi ya marekani kama tukio pekee la
utekaji wa anga (hijacking) ambalo limeshindikana
kufikia hitimisho.
Kwa hivi sasa katika maeneo mbalimbali nchini
marekani na hasa eneo la Airel, mjini Washington
kila mwaka mwezi November watu husherehekea
'Cooper day' kukumbuka tukio hilo la kihistoria
nchini marekani lilotekelezwa na binadamu mmoja
peke yake ambaye kutokana na ustadi alioutumia
kufanikisha azma yake amebakia kwenye vitabu vya
historia, na umahiri wake umemfanya kugeuzwa
kutoka kuwa binadamu wa kawaida mpaka kuwa
'binadamu wa kusadikika'! Mwenyewe alijitambulisha
kama D.B Cooper!

Post a Comment

0 Comments