Ujumbe wa Tamwa kwa Waandishi wa Habari Juu ya Ugonjwa wa Korona




Aprili 11, 2020.Wakati huu ambapo dunia nzima inapambana na ugonjwa wa Covid -19 unaosababishwa na virusi vya Corona, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinawakumbusha wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari kufuata miongozo ya kutekeleza majukumu yao kwa kujilinda na maambukizi ya ugonjwa huu, na kutumia zaidi teknolojia ya mawasiliano.
Ugonjwa wa Covid-19 unaweza kumuathiri mtu yeyote, hivyo wanahabari, wamiliki wa vyombo vya habari na wadau wote wa habari wanapaswa kukubaliana na mabadiliko ya kiutendaji kazi yatakayowaepusha dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu.
TAMWA inawashauri wanahabari na wamiliki wa vyombovya habari kujikita katika kutumia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kupata habari badala ya kwenda katika mikusanyiko isiyo ya lazima kwani taarifa zinaweza kutumwa kimtandao au mahojiano kwa njia ya simu.
“Bila shaka hofu ya ugonjwa wa Covid 19itabadili mfumo wa utendaji kazi wa tasnia ya habari kama taasisi inayohudumia jamii na kuanza kujiona kuwa na wao pia ni sehemu ya jamii,
TAMWA tunathamini usalama wa wanahabari kwa kuwa sisi ni sehemu na mdau wa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa chanzo cha ufikishaji wa taarifa za kutetea haki za wanawake na watoto zenye lengo la kuwa na Tanzania inayoheshimu misingi ya usawa wa jinsia.
Wanahabari wanaoripoti kuhusu COVID-19 na wanahabari wengine, wanashauriwa kufanya maandalizi kabla ya kwenda katika mikutano, kwa kufuata mbinu za kujikinga na maambukizi.



TAMWA tunawatahadharisha wanahabari kuzingatia yafuatayo wanapotekeleza majukumu yao ya kikazi:
·Kuvaa barakoa na glovu za kujikinga ikiwa unafanyia kazi au kutembelea eneo lililoathirika na maambukizi, kama vile kituo cha matibabu, karantini. Vifaa vinginevyo vya kujikinga kama vazi linalositiri mwili wote huenda likahitajika.

·Ikiwa unafanyia kazi katika kituo cha afya, sokoni, au katika maeneo yenye mikusanyiko usithubutu kuweka vifaa vyako sakafuni. Hakikisha umevisafisha vifaa vyako kikamilifu ili kuondoa viini vya maambukizi.

·Daima hakikisha unanawa mikono yako kikamilifu kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono kabla, wakati na baada ya kuondoka katika eneo lenye mkusanyiko.
·Tunaiomba Wizara ya Habari, kutoa mwongozo kwa wanahabari wa namna ya kutekeleza majukumu yao.
·Wamiliki na wahariri ndani ya vyombo vya habari kuzingatia usalama wa wanahabari kwanza kabla ya kuwapangia kazi.Aghalabu wanahabari ni nguzo muhimu ya kuhabarisha umma wakati wa mlipuko wa magonjwa, vita, maafa na ajali, hivyo usalama wao ni muhimupia.
TAMWA inavipongeza vyombo vya habari kwa kuendelea kuhabarisha na kuilekeza jamii kuhusu mwenendo wa janga la Corona. Tanzania bila Corona inawezekana!
 Rose Reuben  
Mkurugenzi Mtendaji  
TAMWA.

Post a Comment

0 Comments