Kwakua
tumetoka kwenye wiki ya mama duniani, niliona si vibaya nikifululiza
habari za wanawake katika thread zangu. Kabla wenzangu hawajanijia juu,
leo naomba niwape ya dada huyu. Usiongee maneno ya kumdharau kwa
mwanamke kabla haujayasikia ya mwanadada Josina Muthemba Machel. Mama wa
Taifa la Msumbiji.
Alipambana
hasa kuifanya nchi yake ipate uhuru lakini uhuru wenyewe hakuuona.
Josina alifariki dunia Aprili 7, 1971, ikiwa ni miaka minne kabla ya
nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka 1975.
Jina
lake ni jina muhimu katika historia ya Msumbiji. Ni kama watanzania
wanavyomtaja Bibi Titi. Lakini jasho na machozi ya Bibi Titi, vimeishia
kwenye kipande cha barabara kutoka Mnazi Mmoja mpaka makutano ya
Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Ohio. Kipande hicho kinaitwa barabara
ya Bibi Titi. Eti hiyo tu ndiyo heshima yake pekee kwa mengi aliyofanya.
Kuna mwenzangu alizungumza maneno haya na sio mimi
Turudi
kwa dada yetu Josina na hayo mengine tutayajadili baadae. Ni mwanadada
aliyethubutu kushika silaha dhidi ya utawala wa Kikoloni wa kireno
akiwahamasisha wanawake wengine pamoja na wanaume kuingia vitani kudai
uhuru.
Josina Muthemba
ambaye baada ya kufunga ndoa aliitwa Josina Machel. Aliolewa na
mwanamapinduzi na aliyekuwa rais wa kwanza wa msumbiji SAMORA MACHEL.
Josina Alizaliwa akiwa pacha na mwenzake Belmiro Muthemba Agosti 10, 1945
Kusini mwa Msumbiji kwenye mji wa Vilanculos, Inhambane. Wakilelewa na
babu ambaye alikua muinjilisti na baba ambaye alifanya kazi kama muuguzi
katika hospitali mbalimbali za serikali.
Alipata
kuingia shuleni akiwa na umri wa miaka 7, Masomo yake alianzia kwenye
mji wa Mociboa da Praia, uliopo Kaskazini ya Msumbiji, baadaye alihamia
kwa bibi yake, Mji Mkuu wa nchi hiyo, Lourenco Marques ambao kwa sasa
unaitwa Maputo.
Familia ya
Josina ilikuwa ikipata upendeleo maalum kutoka kwa wakoloni lakini hilo
halikuifanya familia yake iwasaliti raia wenzao. Mfumo huo uliitwa
Assimilados kwa kireno na kingereza assimilation.
Baada
ya kufkisha miaka 13 alifanikiwa kusoma elimu ya sekondari katika shule
ya biashara ambapo alijiunga na Umoja wa Wanafunzi wa Sekondari nchini
Msumbiji (NESAM) ambao Mondlane alisaidia kuujenga mwaka 1949. Ni umoja
ambao ulilenga kukuza wanafunzi kifikra na kuwajengea uzalendo na moyo
wa kuitetea nchi yao.
Baada ya miaka mitano alifaanya jaribio la kwanza la kutoroka Msumbiji ili kujiunga na chama cha ukombozi wa nchi hiyo, FRELIMO, nchini Tanzania. Miongoni mwa watu waliotoroka na Josina ni aliyewahi kuwa rais wa msumbiji , Armando Guebuza.
Baada
ya kutembea kwa kwa umbali wa maili 800, Josina na wenzake walikamatwa
na wakoloni wa Uingereza katika eneo la Maporomoko ya Victoria Zimbabwe,
kisha wakarejeshwa Msumbiji kwa wakoloni wa Kireno, mjini Maputo.
Alikaa jela na kutoka baada ya miezi mi 5 na kuruhusiwa kuendelea na
masomo yake ya sekondari lakini kwa uangalizi mkubwa wa askari.
Kwakua
alikua mdogo (miaka 19) walimdharau na kuona hawezi fanya lolote hivyo
wakamwacha. Akafanikiwa kutoroka tena akiwa na wanafunzi wenzake. Safari
hii walifika mpaka Swaziland na kupokelewa na baadhi ya wasamaria
katika kambi ya wakimbizi. Walitoroka tena Swaziland yeye na wenzake
watatu baada ya kupata taarifa kuwa wanataka kurudishwa kwenye mikono ya
wareno.
Walisafiri kwa
gari na sehem zingine walitembea kwa miguu mpaka wakafika Johannesburg
South Afrika. Baadaye kikundi hicho kilisafiri kwa lori kwenda
Francistown, Botswana ambapo walijiunga na wengine 14 ambao pia walikua
na lengo la kufika Tanzania. Walikamatwa kama wazamiaji na serikali ya
uingereza, lakini Mondlane akiwa Rais wa Frelimo aliwapambania mpaka
wakakubaliwa kusafiri mpaka Tanzania.
Baada
ya safari ndefu na ngumu katika mabasi ya umma, kundi hilo lilifika
jijini Dar es salaam, Tanzania. Josina alisafiri karibu maili 2,000
kutoka nyumbani kwake.
Josina
akiwa na umri wa miaka 20, aliteuliwa kuwa msaidizi wa mkurugenzi wa
Taasisi ya Msumbiji jijini Dar es Salaam. Taasisi iliyojikita na masuala
ya elimu chini ya mkurugenzi mkuu mama Janet Mondlane, mwanamke wa
Kimarekani, aliyekuwa mke wa Mondalne.
Josiana
aliikataa nafasi ya kujiunga na chuo kikuu nchini Swaziland na kukubali
kujitolea katika taasisi mpya iliyoanzishwa na FRELIMO taasisi ya
Women’s Detachment. Ikiwa na Lengo la kuwahamasisha wanawake kuunga
mkono harakati za ukombozi wa nchi ya Msumbiji.
Mwaka 1967 akiwa mjumbe wa Kamati Kuu ya FRELIMO,
alikuwa mmoja kati ya wanawake waliokwenda Nachingwea mkoani Lindi
kusini mwa Tanzania katika kambi ya mafunzo ya kijeshi. Samora Machel,
rais wa kwanza wa Msumbiji na mume wa baadaye wa Josina alisimama kama
mkurugenzi mkuu wa kituo hiko .
Josina
aliifanya kazi ya kuhubiri matumaini na kuwahamasisha wananchi
kulipigania taifa lao. Alipita kwenye majimbo na kuhamasisha watu hasa
vijana, vilevile alipita kanda za ukombozi na kuhudumia majeruhi.
Mwaka
1968, Josina aliona uhitaji wa vituo vya afya, shule na vituo vya
kulelea watoto katika maeneo ya ukombozi ili kuhudumia watoto waliokuwa
wakipoteza wazazi kutokana na vita.
1969
ulikua mwaka mzuri kwa Josina. Aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Mambo
ya uhusiano ya FRELIMO nafasi ambayo ilimfanya awe anatembea kwenda nchi
mbalimbali kwenye mikutano iliyohusu haki za wanawake.
Ambapo
aliendeleza kwa bidii vituo vya utunzaji wa watoto kaskazini mwa
Msumbiji (Cabo Delgado ) na kutetea watu wa eneo hilo bila kusahau
kuwafundisha umuhimu wa kupeleka wasichana shuleni. Wakati ambao Rais wa
FRELIMO EDUARDO MONDLANE anauawa nchini Tanzania na maajenti wa kireno ili kudhorotesha harakati za ukombozi.
Josina
alikuwa mtetezi wa wanawake kiuchumi, kijamii na kielimu. Alifunga ndoa
na Samora katika Kituo cha Mafunzo cha wilaya ya Tunduru kusini mwa
Tanzania. Novemba mwaka huo alijifungua mtoto wao wa kiume, Samito AKA
Samora Jr
Mwaka
1970 Josina alianza kupata maumivu ya tumbo na kuwa dhaifu ki afya.
Alisafiri na kwenda Moscow kwa matibabu na kuonekana ana saratani ya
ini. Alitakiwa kupumzika lakini Josina alirudi kwenye majukumu yake na
FRELIMO.
Mwisho wa mwaka,
alimuacha Samito na rafiki yake na kuchukua safari ya miezi miwili
ambapo kwa kiasi kikubwa alitembea kwa miguu kupitia Mkoa wa Niassa
kukagua hali na kupanga shughuli mbalimbali kwenye idara yake.
Mnamo
Machi 1971 Josina alisafiri tena, wakati huu alikwenda Cabo Delgado,
kukagua mipango ya kijamii inayotekelezwa huko. Kwa wakati mmoja
alifanya kikao na watu zaidi ya 1000 akiwa mchovu na dhoofulhalia. Hapo
anaamua kurudi Dar es salaam mwanzoni mwa Aprili. Wakati anavuka mpaka
wa Tanzania, alikabidhi bastola yake kwa mwenzake na kumwambia
"Wenzangu, siwezi kuendelea tena. Toa hii kwa kamanda wa jeshi ili iweze
kuchangia wokovu wa watu wa Msumbiji. "
Aprili
5 Josina alikua na hali mbaya mkoani Dar es salaam. Alipelekwa katika
Hospitali ya Muhimbili ila alifariki mnamo Aprili 7, 1971 akiwa na miaka
25. Chama cha FRELIMO kiliitangaza siku hii kuwa siku ya kitaifa ya
wanawake Msumbiji. Ilikuwa ni miaka minne baadae ambapo uhuru
ulipatikana. Alizikwa kwenye kaburi la Kinondoni ambapo alizikwa karibu
na mjomba wake Mateus Muthemba, aliyeuliwa na mawakala wa Ureno mnamo
1968.
Mwaka
1972, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Josina kufariki dunia, mmoja wa
viongozi wa Frelimo, Oscar Monteiro, alimtaja Josina kama kamanda muhimu
wa Frelimo na Msumbiji aliyeangukia njiani. Kauli hiyo ilimfanya Samora
aanguke chini na kulia.
Samora
aliandika shairi kumlilia Josina: “Yaani zaidi ya mke, ulikuwa dada
kwangu, rafiki na kamanda katika jeshi. Tunawezaje kumuomboleza kamanda,
lakini kuchukua bunduki iliyoanguka na kuendelea kupigana. Machozi
yangu yanatiririka kutoka pale kwenye chanzo kilichozaa penzi letu, nia
yetu na mapinduzi ya maisha yetu.”
0 Comments