Ni
ajabu sana hii dunia ilivyoumbwa, umewahi ona wanawake wapambanaji?
Mwanamziki kutoka Kingstone Jamaica Orville Richard almaarufu kama
Shaggy, ana nyimbo yake ambayo amemwelezea mwanamke alivyo na nguvu na
upendo.
Mwanamke
akikaa sehemu basi lazma mambo yanyooke.. kama utahitaji kujadili
kuhusu hili me nipo tayari kukupa mifano ya wanawake wenye sifa hizo.
Dr Hellen Kijo Bisimba nimekupa, Wangari Mathai kutoka Kenya nimekupa, Bibi Zura Karuhimbi kutoka Rwanda nimekupa
na leo nakupa ya Yaa Asantewaa.
Yaa
Asantewaa alikuwa malkia mashuhuri wa Ashanti mwanzoni mwa karne ya
ishirini ambaye bado ni ishara ya nguvu mpaka leo hii. Inasadikika
alizaliwa kati ya miaka ya 1840 hadi 1860 huko Ashanti ambapo ndio
Ghana ya leo. Alikuwa mkulima mzuri kabla ya kuwa mama Malkia mnamo
miaka ya 1880. Inaaminika kuwa alichaguliwa na kupewa cheo hiki na kaka
yake mkubwa Nana Akwasi Afrane Okpase, ambaye alikuwa mtawala mwenye
nguvu wakati huo.
Kama
Mama Malkia, Asantewaa alishikilia majukumu mengi, ikiwa ni pamoja na
kuwa mlinzi wa kiti cha dhahabu. Kiti cha dhahabu ni ishara ya ufalme wa
Ashanti, mfumo wa kitamaduni, na nguvu. Yeye ndiye anakuwa mshauri mkuu
wa Mfalme, na kuifanya nafasi yake kuwa ya pili kicheo kutoka kwa
mfalme na ni jukumu lake kukilinda kiti hiko.
Mnamo
1896, watu wa Ashanti walianza kupambana na muingereza katika nchi yao
ikiwa ni jaribio la Uingereza kujenga koloni katika nchi ya Ghana. Ili
kulipiza kisasi, Waingereza walimteka na kumfukuza Asantehene Prempeh I,
Mfalme wa Ashanti na mjukuu wa Asantewaa Kofi Tene, ambaye pia alikuwa
kiongozi mwenye nguvu. Waingereza waliondoa mfalme na viongozi wengine
wa Ashanti na kuwapeleka Visiwa vya shelisheli ili waweze kupata kiti
cha dhahabu.
Sir
Frederick Hodgson wa Gold Coast alifikiri ya kwamba ugumu wa kutawala
Waashanti ungepungua kama yeye mwenyewe angeshika kiti cha dhahabu.
Wanajeshi aliotuma kukitafuta walishindwa. Hivyo gavana Hodgson mwenyewe
alienda Kumasi akaita mkutano wa watawala wa maeneo ya Ashanti akadai
kupewa kiti cha dhahabu na malipo ya kodi.
Hotuba
ya gavana ilikasirisha viongozi lakini waliondoka kimya. Yaa Asantewaa
alishiriki na kabla ya mkutano alionekana kumtania gavana kwa kusimama
mbele yake na kuangalia nishani kwenye sare yake kwa muda mrefu.
Baada
ya kusikia madai ya gavana alimpinga kwa kumwambia hastahili kupata
kiti cha dhahabu na akikitaka amrudishe Asantehene anayejua maficho ya
kiti hiko.
Walikutana
baadaye kati yao wakishauriana namna gani kujibu mapigo ya mwingereza.
Yaa Asantewaa Alipoona ya kwamba sehemu ya viongozi walitaka kunyamaza
alitoa hotuba akiwauliza wakuu wengine namna gani waliweza kunyamaza tu
na kuyanyamazia maneno ya Mwingereza, na kama wameacha kuwa wanaume ili
wabadilishwe kuwa wanawake? Asantewaa alitangaza kwamba ikiwa wanaume wa
ufalme hawatatetea watu, basi wanawake wataibuka. Hee kauli nzito hizi,
ukitaka kuona nguvu za wanaume toa kauli kama hizi.
Katika
mkutano huu Yaa Asantewaa alichaguliwa kuwa kiongozi wa vita wa
Ashanti. Asantewaa alishikilia msimamo wake na kuwasaidia askari.
Alisimama kama Kamanda Mkuu wa jeshi la Ashanti. Na kupelekea vita vya
tano na vita vya mwisho vya Anglo-Ashanti dhidi ya muingereza
vilivyojulikana kama Vita vya Uhuru vya Yaa Asantewaa (au Vita vya kiti
cha Dhahabu), ambavyo vilianza Machi 28, 1900.
Yaa
Asantewaa aliongoza uasi ambao ulisababisha vifo cha wanajeshi 1,000 wa
Uingereza na washirika wa Kiafrika na Ashanti 2000.Hii ilikua idadi
kubwa kuwahi kutokea katika vita vyote ambavyo vilipita .
Vita
iliendelea hadi Julai ambapo Waingereza walikusanya jeshi jipya kutoka
vikosi vyao vya Sierra Leone na Nigeria na jeshi hili lilifika Kumasi
kwenye Julai na kufukuza jeshi la Waashanti. Katika miezi iliyofuata
walishinda upinzani wote.
Yaa
Asantewa ni mfano muhimu na msukumo kwa wasichana na wanawake wengi
nchini Ghana na afrika kwa ujumla kwasababu ya ujasiri aliouonyesha.
Wanawake wengi ambao wanafanya kazi ambazo hapo awali zilikuwa
zikitawaliwa na wanaume mara nyingi wamepewa jina la Yaa Asantewaa ikiwa
ni njia ya kuwatia moyo na kuwaunga mkono.
Mnamo
mwaka 2000, makumbusho moja ilijengwa kwa kumbukumbu ya malkia huyo wa
vita huko Ejisu. Familia yake ilikuwa na ukarimu wa kutosha kuchangia
vitu maalum vya urithi na vitu ambavyo Yaa Asantewaa alivitumia, ikiwemo
nguo, gamba la kobe ambalo inaaminika alikuwa akitumia kulia chakula.
Kwa bahati mbaya, makumbusho hayo yaliungua kwa moto Julai 2004. Vitu
vingi vilipotea na makumbusho hayo yamesalia tupu.
0 Comments